BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MBUNGE WA NKASI KUMBE HAMWOGOPI BOSI WAKE WAZIRI MKUU PINDA, AFICHUA SIRI ZA NDANI ZA KAMATI NAMBA MOJA KATIKA KIKAO VYA BUNGE LA KATIBA MCHANA KWEUPE DODOMA.

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Ali Mohamed Kessy ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM) akiwatangazia waandishi wa habari kuunga mkono muundo wa serikali tatu uwepo katika Katiba Mpya, mjini Dodoma jana. Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati namba moja ya bunge hilo, Ummy Mwalimu na Makamu wake, Prof Makame Mbarawa ambao walimwita Kessy kumtaka kukanusha kuhusu taarifa yake ya kuwapo tatizo la akidi kwenye vikao vya kamati. Picha na Emmanuel Herman
 

Dodoma. Jana ilikuwa kama sinema pale viongozi wa Kamati Namba Moja ya Bunge Maalumu walipojikuta wakibishana na mjumbe wao mbele ya waandishi wa habari, huku siri za mambo ya ndani ya vikao zikianikwa hadharani.

Kamati hiyo inaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu na makamu wake ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, huku ikiwa imesheheni vigogo wengine wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.


Viongozi wengine katika kamati hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uhusiano na Uratibu), William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.


Wamo pia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.


Jana asubuhi, Mwalimu na Profesa Mbarawa walifika mbele ya waandishi wa habari katika Hoteli ya St Gasper wakiwa wameambatana na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy.


Lengo la mwenyekiti na makamu wake lilikuwa ni kumbana Keissy ili akanushe taarifa aliyoitoa juzi kwenye moja ya televisheni kwamba kamati hiyo inaongoza kwa kuvunja kanuni hasa katika suala la akidi ya vikao kutotimia.


Sinema ilivyoanza
Walipofika mbele ya waandishi wa habari, Keissy alipewa fursa ili akanushe taarifa yake, lakini alibadili mada na kuanza kuzungumzia masuala ya muundo wa Serikali na Bunge, huku akisema yeye ni muumini wa serikali tatu na siyo mambo ya serikali mbili zinazopendekezwa na wengi kutoka katika chama chake.


Kauli hiyo iliwashtua Mwalimu na Profesa Mbarawa ambao walianza kumkatisha ili asiendelee.


“Keissy sikukuitia mambo hayo, huu ni mkutano wangu, naomba ukanushe nilichokuitia, hayo utazungumza baadaye tafadhali sana,” alisema Mwalimu.


Wakati huo Profesa Mbarawa na waandishi wa habari waliokuwapo walivunjika mbavu kwa vicheko, huku yeye akiendelea kusisitiza kwamba ni muumini wa Tanganyika.


Wakati akisema hayo, Profesa Mbarawa naye aliingilia kati na kumtaka Keissy kueleza kilichompeleka hapo huku akimtaka aache kelele za kupotosha wananchi kwa kuwa anachosema siyo kweli.


Alipopewa nafasi ya kuzungumzia jambo hilo, Keissy alisema: “Jana (juzi), mimi nilihesabu mara mbili nikaona Zanzibar hawajatimia lakini kumbe mmoja nilimfanya akawa mtu wa Tanganyika, kwa hilo nilighafilika, lakini mle ndani mambo siyo mazuri,” alisema Keissy.


Kabla hajaendelea Mwalimu alidakia na kumtaka anyamaze kimya kwa kuwa huo haukuwa mkutano wake, ili yeye (Mwalimu) aendelee kueleza mambo yaliyojiri ndani ya kamati.


“Jamani waandishi si mnaona amekanusha, huu ni mkutano wangu na yeye sitaki azungumze mambo ya mle ndani kwa kuwa msemaji ni mimi au makamu wangu au mtu yeyote atakayeteuliwa na mwenyekiti, sasa tunaendelea,” alisema Mwalimu.


Mara baada ya Mwalimu kutoa taarifa ya kamati yake kwa waandishi wa habari na kumaliza kujibu maswali, alinong’ona na Profesa Mbarawa na hapo wakampa nafasi Keissy ili azungumze kwa ufupi mambo yake lakini palepale mbele yao.


Kauli za Keissy
Akitumia fursa hiyo, Keissy alisema: “Kuna mambo yanafanywa mle ndani ambayo mimi na wenzangu wengine tunalazimishwa, hatukubaliani nayo likiwamo suala la kuizika Serikali ya Tanganyika wakati wa upande wa pili (Zanzibar) wanapewa nafasi na kunufaika na rasilimali za nchi hii, ndugu zangu huu ni uonevu.”


Alisema uonevu huo umekuwa mkubwa kwa wabunge wa Tanzania Bara ukilinganisha na wenzao wa Zanzibar ambao alisema wanakula fedha nyingi za bure ilihali hawafanyi kazi za Tanganyika.


“Ndugu zangu, hapa tusidanganyane, we fikiria watu zaidi ya 50 wanatoka kule Zanzibar na kuja kutuamulia mambo yetu, hii si halali hata kidogo. Haiwezekani mtu wa Zanzibar akaja kuzungumzia masuala ya Nkasi wakati hayajui,” alisema.


Alisema kuwa msimamo wake siku zote ni serikali tatu na kwamba hatayumbishwa na vitisho au jambo la aina yoyote hata kukiwa na kulazimishwa.


Mbunge huyo alisema kuwa kutakuwa na urahisi wa kuongoza Serikali kama Tanganyika itapewa hadhi yake kuliko ilivyo sasa kwa serikali mbili zinazopigiwa upatu.


Kwa mapendekezo yake alisema ni vyema likawepo Bunge la Tanganyika, Bunge la Zanzibar na kisha miongoni mwa wabunge hao, wachaguliwe wachache kuunda Bunge la Muungano.


Aliendelea kusisitiza kuwa wabunge kutoka Zanzibar wanawanyonya wenzao wa Tanzania Bara kwa kila kitu kauli ambayo ilionekana kumkera Profesa Mbarawa na kuamua kumkatisha asiendelee kuzungumza.


Wakati akiendelea kuzungumza, viongozi hao walimkatisha tena na kumwambia akubali waondoke pamoja kuendelea na vikao vya kamati. Baada ya hapo, Mwalimu na Profesa Mbarawa walinyanyuka na kuanza kuondoka, lakini Keissy alisimama na kuendelea kuzungumza na waandishi wa habari.


Baada ya kuona anaendelea, Profesa Mbarawa alirudi na kumshika mkono Kessy huku akisema; “Mheshimiwa Keissy twende bwana, maana ukimwacha huku huyu atazungumza mambo mengi.”


Wakati akiondoka eneo hilo, Keissy alipaza sauti akiwaambia waandishi wa habari: “Angalieni tunavyodhibitiwa, lakini msimamo ni huo wala sitayumba ngoja tukaendelee lakini mimi ndiyo mtoa habari namba moja.”


Msimamo wa serikali tatu ni wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) waliosusia Bunge.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 comments:

Anonymous said...

aliyekwambia bosi wa mbunge ni waziri mkuu ni nan acha ulimbukeni