BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VIONGOZI WA UAMSHO WAWAZULIA JAMBO POLISI KUWA WALITUMIA USHENZI NA UKATILI WAKATI WAKIWAHOJI..

Wanachama wa kundi la uamsho wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wakitoka wakiwa chini ya ulinzi wa Magereza walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory
 

Dar es Salaam. Viongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), akiwamo Sheikh Farid Hadi Ahmed (43) wameilalamikia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa polisi “walitumia ushenzi na ukatili” wakati wa kuwahoji.

Farid na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kuwaingiza watu nchini kushiriki katika vitendo vya ugaidi, kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo hivyo.


Washtakiwa hao walitoa malalamiko hayo jana kwa Hakimu Mkazi, Hellen Liwa muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali, Peter Njike kuiomba Mahakama iwaruhusu washtakiwa saba kwenda polisi kuhojiwa kwa ajili ya upelelezi zaidi.


Baada ya wakili huyo kuwasilisha ombi hilo, Sheikh Farid aliuliza: “Wametuomba tena kwenda kuhojiwa? Kwanza waliotuhoji hawakutumia ustaarabu wala ubinadamu ilikuwa ni ushenzi na ukatili. Walituhoji wakati tukiwa watupu na kutupiga”.


Sheikh Farid alidai kuwa kiongozi Mkuu wa Jumuiya za Uamsho, Sheikh Mselem Ali Mselem alimweleza watu hao walichomfanyia.


Hata hivyo, Hakimu Liwa alimwambia alimtaka kuzungumzia kile ambacho amekiona siyo cha kusimuliwa.


Aliendelea kueleza: “Walipigwa na wala hawakupewa matibabu na watu wameumizwa, utakuta wanakojoa damu wiki moja hadi mbili, tunaomba wafanyiwe uchunguzi wa afya zao.”


Mshtakiwa Salum Ali aliiomba Mahakama kupeleka daktari mahabusu kwa madai kuwa wanafanyiwa vitendo vya ‘kuingiliwa kinguvu’ na kuhoji kwa nini wamekamatwa Zanzibar na kushtakiwa Bara wakati waliokamatwa Arusha walishtakiwa hukohuko na hawakupelekwa Dar es Salaam au Zanzibar?


Akiendelea kutoa malalamiko yake, Sheikh Farid alidai kuwa wao wamekamatwa kwa sababu hawautaki Muungano na kwamba huo ndiyo msingi wa kesi hiyo.


Baada ya kauli hiyo, Hakimu Liwa alisema: “Tupo kwenye mchakato wa Katiba Mpya na masuala ya muungano yanatajwa mbona watu wanasema na hawakamatwi?”


Mara baada ya Hakimu Liwa kusema hayo, Sheikh Farid alidai ni kwa sababu wao wanahubiri ukweli na watu wanaukubali.


Hakimu Liwa aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 3, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.


Katika kesi hiyo, Sheikh Farid na Jamal Nooridin Swalehe (38) waliunganishwa na wenzao 18 mahakamani hapo.


Mbali na Sheikh Farid na Jamal, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni Nassoro Hamad, Hassan Bakari, Ahtari Humoud, Mohamed Isihaka, Abdallah Hassan, Hussein Mohamed, Juma Sadala, Said Kassim, Hamis Amour, Abubakar Abdallah, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Othman, Rashid Ally, Amir Hamis, Kassim Salum na Said Shehe.


Kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Januari 2013 na Juni, mwaka huu walipanga njama ya kutenda makosa hayo na kuwezesha kufanyika kwa vitendo vya kigaidi.


Katika kipindi hicho na maeneo tofauti nchini, Sheikh Farid anadaiwa kuwa aliwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.


Pia Sheikh Farid anadaiwa kuwa kwa makusudi na akijua kuwa anatenda kosa alitoa msaada kwa watu hao kutenda vitendo vya kigaidi kinyume cha sheria na anadaiwa kuwa katika kipindi hicho akiwa anajua kuwa Sadick na Farah wametenda makosa ya kigaidi, aliwahifadhi.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: