BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

JOHN MNYIKA ABEBESHWA MIKOBA YA ZITTO KABWE NDANI YA CHADEMA.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemteua tena Dk Willibrod Slaa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani kwa sasa nchini. Hii ina maana kwamba Dk Slaa mwenye umri wa miaka 65, atashika wadhifa huo hadi mwaka 2019. Alianza kushika nafasi hiyo mwaka 2002, akitoka kuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, nafasi aliyoishika kuanzia mwaka 1998.

Matokeo hayo yalitangazwa jana na Msimamizi wa Uchaguzi wa Chadema, Dk Steven Kimondo.

Alisema uteuzi huo, ulipendekezwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na kupata baraka za Kamati Kuu ya chama hicho.

Wakati Dk Slaa akiteuliwa kuendelea kushika wadhifa huo, Kamati Kuu ilithibitisha uteuzi wa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Tanzania Bara.

Mbowe, ambaye usiku wa Jumapili alichaguliwa kwa kishindo kukiongoza chama hicho kwa awamu ya tatu ya miaka mitano, pia alimteua mtangazaji maarufu nchini, Salum Mwalim kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, ambaye naye amethibitishwa kushika wadhifa huo.

Uteuzi huo wa Katibu Mkuu na manaibu wake, unaifanya safu ya viongozi wakuu ndani ya chama kukamilika. Usiku wa Jumapili, wajumbe wa mkutano mkuu wa Taifa wa Chadema mbali ya kumchagua Mbowe, pia uliwachagua makamu wawili, Profesa Abdallah Safari kwa upande wa Tanzania Bara na Said Issa Mohammed kwa upande wa Zanzibar.

Kabla ya uchaguzi wa Jumapili, wajumbe hao waliwachagua Hashim Juma Issa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema, na Makamu wake ni Susan Lyimo kwa upande wa Tanzania Bara na Omar Masoud Omar kwa upande wa Zanzibar.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ndiye Mwenyekiti mpya wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), wakati Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Mwenyekiti wake ni Paschal Patrobas na atasaidiwa na Makamu wake, Patrick Ole Sosopi (Bara) na Zuedi Abdulahi (Zanzibar).

Uteuzi wa safu hiyo mpya ya uongozi, unamtupa moja kwa moja kiongozi kijana na mwenye ushawishi wa kisiasa, aliyekuwa akishika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara, Zitto Kabwe ambaye kwa sasa ana mgogoro na chama hicho.

Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alituhumiwa kuhujumu chama hicho kiasi cha uongozi kutangaza kumvua nyadhifa zote ndani ya chama, hatua iliyopingwa kisheria na mbunge huyo, kwani alifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akiitaka mahakama iizuie Chadema kujadili uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.

Katika kesi hiyo inayoendelea, Zitto atetewa na Wakili Albert Msando na Chadema inawakilishwa na mawakili wawili, Tundu Lisu na Peter Kibatala.

Kadhalika, anaoimba mahakama imwamuru, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willibrod Slaa kumkabidhi nakala za taarifa na mwenendo mzima wa vikao vilivyomvua uongozi ili akate rufaa katika ngazi ya juu ya chama hicho.

Zitto kupitia wakili wake, Msando aliomba mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu na vikao vingine vya chama, kutojadili suala la uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Akiwasilisha hoja zake, Msando aliomba zuio hilo litolewe hadi Zitto atakapopata nafasi ya kuwasilisha rufaa yake ya kupinga uamuzi wa kumvua uongozi katika chama, uliotolewa katika kikao kilichofanyika Novemba 12 mwaka 2013.

Wakili huyo alidai endapo amri hiyo haitatolewa na Kamati Kuu ikamvua uanachama, Zitto atapata athari kubwa kuliko chama chenyewe, kwa kuwa atapoteza nafasi yake ya ubunge na kushindwa kuwatumikia wananchi waliomchagua.

Pia, mwanasheria huyo alidai athari nyingine ni kwamba iwapo atafukuzwa uanachama, Zitto atapoteza nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Alisisitiza kuwa Zitto haizuii Chadema kufanya kazi zake za kisiasa, kama wao wanavyodai katika hati ya kiapo kinzani, bali anaomba Kamati Kuu isijadili suala lake la uanachama mpaka uamuzi utakapotolewa.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: