BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DIAMOND ASALIMISHA KOMBATI ZAKE ZA KIJESHI HUKU UWOGA UKIWA UMEMJAA MOYONI KATIKA KITUO CHA POLISI


Mwanamuziki Diamond akitumbuiza kwenye tamasha la fiesta mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye viwanja wa Leaders Club. Picha na Bongo5.com

Dar es Salaam.
Mwanamuziki Nassib Abdul, ‘Diamond Platnumz’ amesalimisha nguo zake za kijeshi kwenye Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.


Diamond alisema kuwa juzi alipokea wito uliomtaka afike kituoni hapo (Oysterbay) akiwa na madansa wake pamoja na nguo hizo. Alisema haikuwa rahisi kwake kutii amri ya vyombo vya dola kwani alikuwa na woga kutokana na kutokuwa na rekodi ya yoyote ya matukio ya uhalifu.


“Nisingeweza kukaidi amri ya dola, nilifika na yale mavazi na nikahojiwa kwa saa kadhaa. Nikaeleza kwamba yalikuwa yakifanana na ya jeshi na hayakuwa sare rasmi za jeshi hilo, kikubwa nilihitaji kumaliza tatizo,” alisema nyota huyo aliyetajwa kuwania tuzo za MTV EMA zinazotarajiwa kufanyika Novemba 9 mjini Glasgow, Scotland.


Diamond alisema si kweli kwamba alichukuliwa dhamana na Chifu Kiumbe, ila ukweli ni kwamba alisindikizwa na mdau huyo wa sanaa nchini kama kaka yake kutokana na woga aliokuwa nao, lakini hakushikiliwa na kutakiwa dhamana yoyote.


“Awali, meneja wangu (Hamis Tale) alishikiliwa kwa muda na mimi nikatakiwa kufika na zile nguo nikiwa na dansa wangu ambao na wao walivaa pia, nilifanya hivyo na nikafika pale na kuziacha nguo baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika,” alisema.


Diamond alijikuta akiingia kwenye matatizo na Jeshi la Wananchi (JWTZ) baada ya kupanda jukwaani Jumamosi katika onyesho la Fiesta akiwa amevalia nguo zinazofanana na sare za jeshi hilo.


Hata hivyo, Diamond alisema mavazi yale aliyoyavaa siku ile katika tamasha la Fiesta, hayakuwa ya JWTZ kama inavyodaiwa, bali aliyanunua alipokuwa kwenye ziara yake nchini Ujerumani mwezi uliopita.


Wakati huohuo, Diamond ni miongoni mwa wasanii waliopangwa kutoa burudani katika Siku ya Msanii itakayofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, kesho.


Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Siku ya Msanii 2014 inayoandaa sherehe hiyo, Peter Mwendapole alisema Diamond ataungana na Yamoto Band katika kutoa burudani siku hiyo.


“Maandalizi yote yameshakamilika na leo hii namtambulisha kwenu msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Diamond kuwa ni miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika sherehe hizo pale Mlimani City akiwa sambamba na kundi la Yamoto,” alisema Mwendapole.


Kwa upande wake, Diamond amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na tasnia ya sanaa hapa nchini na pia kuwaenzi wasanii wao.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: