BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HOFU YA KUINGIA KWA UGONJWA WA EBOLA KATIKA ARDHI YA TANZANIA YAWAPA KIWEWE WANANCHI.

 
Mganga Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Dk Mtumwa Mwako

SERIKALI imetangaza kuwaweka kwenye karantini wahudumu wote, wanaomhudumia mgonjwa anayesadikiwa kuwa ana dalili za ugonjwa unaofanana na homa ya ebola.


Hali hiyo inatokana na wakazi wa kata ya Shirimatunda Manispaa ya Moshi, kuingiwa na hofu ya kupoteza maisha yao, kutokana na kuwepo kwa mgonjwa huyo aliyelazwa katika zahanati ya kata hiyo.

Serikali pia imechukua tahadhari kuanzia katika familia ya mgonjwa mwenyewe, mke wake aliyepo jijini Dar es Salaam na familia kwa ujumla, magari aliyopanda, maeneo aliyotembelea na kote alipopita, na kuwaondoa wananchi wasiwe na hofu, kwani tahadhari zote zimechukuliwa.

Mbali na kukiri kuwepo hofu hiyo na kuchukua tahadhari, serikali mkoani Kilimanjaro imesema taarifa za awali, zinaonesha mgonjwa huyo hana ebola, bali ana ugonjwa wa malaria kali.

Mganga Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Dk Mtumwa Mwako alisema wataalamu wanaomhudumia mgonjwa huyo, nao wamewekwa katika karantini hadi hapo sampuli za vipimo zitakaporejea, kwamba mgonjwa huyo anasumbuliwa na kitu gani kingine.

Akizungumza na HabariLeo, Daktari wa Manispaa ya Moshi, Christopher Mtamakaya alisema wahudumu wanne wanaomhudumia mgonjwa huyo ndiyo wamewekwa kwenye karantini. Kati yao watatu ni wanawake na mmoja ni mwanamume.

Alisema wataendelea kuwepo kituoni hapo chini ya karantini hiyo hadi hapo majibu ya vipimo ambavyo vimepelekwa Nairobi, Kenya yatakapotoka.

“Iwapo itabainika mgonjwa ana ebola wahudumu wataongezewa siku 21 za kuendelea kuwepo kituoni kumhudumia mgonjwa na iwapo vipimo vitaonesha mgonjwa hana ebola Jumatano ijayo kituo cha afya kitafunguliwa na huduma kuendelea kama kawaida,” alisema.

Mgonjwa huyo aliyewekwa karantini katika Zahanati ya Shirimatunda ni mwanamume mwenye miaka 37, anayefanya biashara zake nchini Senegal. Wataalamu wameshachukua sampuli za vipimo, kuthibitisha kama ni malaria pekee ama la.

Mkuu wa Mkoa huo, Leonidas Gama alisema wataalamu wa afya katika manispaa hiyo walimgundua mgonjwa huyo Oktoba 22 na tayari sampuli za vipimo zimepelekwa Dar es Salaam na baadaye Nairobi, Kenya kuthibitisha kama ugonjwa unaomsumbua ni malaria pekee au la.

“Serikali imeona itoe taarifa sahihi ya nini kipo katika hofu ya ugonjwa huu,tumechukua tahadhari zote,tumemtenga tu ili afanyiwe uchunguzi, nawahakikishia wananchi kuwa hakuna ebola na hata kama ikiwa ni ugonjwa huo, tumejipanga kwa thadhari zote,” alisema.

Gama alisema taarifa kutoka kwa wataalamu zinaonesha kwamba mgonjwa huyo sasa afya yake inaendelea kuimarika, kwani hata homa kali aliyokuwa nayo imepungua na anaendelea vyema.

Dk Mwako alisema ingawa bado majibu ya vipimo vya mgonjwa huyo hayajatolewa, lakini wananchi wapunguze salamu za kupeana mikono na kukumbatiana ili kuepusha zaidi athari za ugonjwa huo kama utaingia mkoani hapa.

“Kuwepo kwa kituo katika zahanati ya Shirimatunda ni kawaida, kingeweza kuwa sehemu yoyote, hata hivyo tunaomba wananchi watupe ushirikiano kama kuna mtu ametoka nchi za Afrika Magharibi waseme ili tumtenge, hata kama hana ugonjwa ili achunguzwe kwanza,” alisema.

Kutokana na hofu hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imelazimika kuifunga kwa muda usiojulikana zahanati hiyo na kuwahamishia wagonjwa katika hospitali nyingine, ikiwamo ya St Joseph katika manispaa hiyo.

Gama alisema Serikali pia imetenga vituo vingine katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Holili na Tarakea wilayani Rombo na Shirimatunda Manispaa ya Moshi kama tahadhari, iwapo atabainika mgonjwa yeyote ndani ya mkoa huo.

“Mkoa wetu ni miongoni mwa mikoa ambayo inapokea wageni wengi kutoka nje ya nchi kwa ajili ya utalii na biashara, nipende kuwahakikishia wao pamoja na wananchi kwamba mkoa upo salama na waendelee kuja na kufanya biashara,” alisema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigongoni, kata ya Shirimatunda ilipo zahanati hiyo, Juma Sambeke aliliambia gazeti hili juzi kuwa maeneo yatakayoathirika zaidi kwa kufungwa kwa zahanati hiyo ni Shirimgungani, Cherereni ya Moshi Vijijini, Karanga, Soweto, Bonite Madukani na mtaa wa Kigongoni.

Zahanati hiyo inahudumia zaidi ya watu 5,000 kwa mwezi.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: