BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MFUKO WA BIMA YA AFYA (NHIF) WAKUMBWA NA KASHFA YA UFISADI WA KUTUMIA FEDHA ZAIDI YA SH 200 MILIONI KUMNUNULIA GARI WAZIRI WA WIZARA.


MFUKO wa Bima ya Afya (NHIF), umekumbwa na kashfa ya ufisadi ya kutumia zaidi ya sh. milioni 200 kununua gari jipya ambalo wamemkabidhi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid.

Pia Bodi ya mfuko huo ambayo hupata fedha kutokana na michango ya wanachama wake, imetumia zaidi ya sh. bilioni mbili katika kipindi kisichozidi miezi sita badala ya mwaka mzima kama ilivyotengewa kwenye bajeti ya mfuko huo kwa mwaka huu wa fedha.

Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumatano, umebaini kuwa gari hilo lilinunuliwa kwa ajili ya matumizi ya Mkurugenzi wa Mfuko huo.

Gari hilo aina ya Nissan toleo jipya kabisa, lenye namba za usajili SU 39931, lilikabidhiwa kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Rashid Oktoba 11, mwaka huu, saa 9.15 na sasa limebadilishwa namba na kuwekwa kibao cha Waziri wa Afya (W AF).

Sababu inayotajwa na NHIF kukabidhi gari hilo kwa waziri huyo ni kwamba gari lake la awali alilopewa na serikali wakati anaingia wizarani, limeharibika na liko kwenye matengenezo.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya mfuko huo, vililiambia gazeti hili kuwa uamuzi wa kulikabidhi gari hilo kwa waziri, ulitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa NHIF, Khamis Mdee ambaye aliwaagiza wafanyakazi wa idara ya rasilimali watu kutekeleza agizo hilo na hakutaka kuulizwa maswali.

Baadhi ya watumishi wa mfuko huo walienda mbali zaidi wakidai kuwa Mdee alitoa gari hilo kwa waziri kama moja ya ushawishi wa kutaka ateuliwe kuwa mkurugenzi mpya wa mfuko, kushika nafasi iliyoachwa wazi na Emmanuel Humba aliyemaliza muda wake.

“Kwa kawaida mawaziri hupewa magari na serikali na hata yakiharibika matengenezo yake yanagharimiwa na serikali, lakini sio kazi ya taasisi yoyote ya umma iliyo chini ya wizara husika kununua gari kwa ajili ya waziri.

“Hivi leo kaimu mkurugenzi wetu akikosea kitu chochote kile, waziri aliyepewa gari hilo atakuwa na uwezo wa kumwajibisha?”alihoji mmoja wa maafisa waandamizi wa mfuko huo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Bodi yatafuna bil.2/-
Kuhusu kashfa ya matumizi ya sh. bilioni 2 katika kipindi kisichozidi miezi sita, uchunguzi umebaini kuwa feha hizo zilitengwa kwa ajili ya bajeti ya Bodi ya wakurugenzi kwa mwaka huu wa fedha.

“Jambo la ajabu ni kwamba, bodi hiyo imetumia fedha hizo ndani ya miezi mitatu tu na sasa inaishi kwa kukopa kutoka kwenye kasma zingine,” alisema mtoa taarifa wetu.

Habari zinasema kuwa bodi hiyo imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kufanya ziara za mafunzo nje ya nchi na zimekuwa zikigharimua mamilioni ya fedha.

Mkuregenzi ajitetea
Kaimu mkurugenzi wa NHIF, Mdee alipoulizwa kuhusu madai hayo, alikiri taasisi yake kukabidhi gari hilo kwa waziri wa Afya, lakini alikana kwamba hatua hiyo haina nia ya kushawishi ateuliwe kuwa mkurugenzi mpya wa mfuko huo.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, alisema huo ni utaratibu wa kawaida na hata utoaji wa gari hilo umezingatia matakwa ya sheria.

Alisema mfuko huo umeamua kukabidhi gari hilo kwa waziri huyo kwani gari lake la awali alilokuwa akilitumia limeharibika na litakapotengamaa gari hilo litarudishwa mikononi mwa NHIF.

“Tuhuma hizo na nyingine zote unazozisikia ni majungu ambayo sijui lengo lake. Huyo ni waziri wetu na taasisi hii ipo chini ya wizara yake. Kuna ubaya gani kumpa gari akalitumia kwa muda wakati anasubiri gari lake?” alihoji Mdee na kusisitiza kuwa hayo ni majungu.

Akijibu madai kwamba ametoa gari hilo kama ushawishi wa kutaka uteuzi wa ukurugenzi, Mdee alisema wenye mamlaka ya uteuzi huo wako juu na hakuna namna mtu anaweza kufanya ushawizi ili ateuliwe.

Baada ya Humba aliyeasisi kuanzishwa kwa mfuko huo, kumaliza muda wake, Bodi ya wakurugenzi ilimteua Mdee kukaimu nafasi ya hiyo.

Serikali ilitangaza nafasi hiyo kuwa wazi na kuwataka wenye sifa kuomba, lakini hadi sasa mchakato wa kumpata mkurugenzi mpya, bado unaendelea. Hata hivyo ni miezi sita sasa imepita tangu kukamilika kwa usaili wa kumtafuta mkurugenzi mkuu mwingine na Mdee anapewa nafasi kubwa.

Kauli ya Wizara
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, Msemaji wa Wizara ya Ujenzi ambayo pamoja na mambo mengine inahusika na suala la magari ya viongozi wa serikali wakiwemo mawaziri, Segolema Francis alisema hawana taarifa na gari la Waziri wa Afya kuharibika na pia hawana taarifa kama Bima ya Afya kutoa gari kwa ajili ya kumsaidia waziri katika kipindi hiki.

“Kweli tunahusika na magari ya mawaziri na watendaji wengine wa serikali, lakini hatujui kama waziri unayemtaja hana gani na ameazimwa la NHIF. Naomba unipe muda nifuatilia suala hilo hadi leo tunalitolea majibu,” alisema.TANZANIA DAIMA.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: