BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

PENDEKEZO LA KUWAPIMA ULEVI MADEREVA WA MAGARI LITEKELEZWE.


By Angela Semaya

AJALI za barabarani zimeendelea kuwa mzimu unaotafuna Watanzania kila siku pamoja na kuwepo juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuhakikisha ajali zinapungua kama sio kutotokea kabisa.

Kuna sababu nyingi zinazopelekea matukio ya ajali ambayo yamekuwa yakichukua maisha ya Watanzania na kuacha wengine wakiwa walemavu.

Moja ya chanzo kikubwa cha ajali ni madereva kuendesha magari wakiwa katika hali ya ulevi, jambo ambalo linasababisha washindwe kuhimili vyombo hivyo barabarani na matokeo yake kugongana ama kugonga watu.

Katika kukabiliana na hilo kamati maalum iliyoundwa na serikali kutathmini ongezeko la ajali za barabarani nchini katika ripoti yake imependekeza madereva watakaokutwa wananuka pombe wafutiwe leseni.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Shio akikabidhi ripoti hiyo kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk, Harrison Mwakyembe na Waziri wa Kazi na Ajira Gaudentia Kabaka alisema Sheria ya Usalama Barabarani inasema mtu asiendeshe huku akiwa amelewa bila kujua ni kwa kiwango gani.

Shio alisema ingawa watu wapo wanaohoji itajulikanaje mtu amelewa bila kupima, ripoti inapendekeza dereva akiwa na harufu tu ya pombe afutiwe leseni.

Pendekezo hilo limetokana na matokeo ya uchunguzi wa ajali nyingi zinazotokea nchini, uliofanywa na kamati hiyo ambapo ilibainika kuwa makosa makubwa yanayosababisha ajali za barabarani ni ya kibinadamu na kubwa ni ulevi.

Mapendekezo ya kamati hiyo yanastahili kuzingatiwa kwa umakini kwa sababu hakuna ubishi ulevi umekuwa ni chanzo kikubwa cha ajali za barabarani ama dereva kujisababishia kifo au ulemavu au kusababishia watu wengine vifo au ulemavu.

Nakubaliana na mapendekezo ya kamati hiyo kuwa watakaokutwa wananuka pombe ni vyema wakafutiwa leseni, nikiamini adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa wale ambao wanaamua kulewa na kuweka rehani maisha ya watu wengine.

Jambo la kusikitisha unakuta dereva amelewa mchana kweupe tena anaendesha gari la abiria na anakwenda safari ya mbali akiwa amebeba watu gari limejaa wakati ajali haina uzoefu wala ujuzi wa dereva barabarani.

Kama itapitishwa adhabu hii ya kuwafutia leseni watakaokutwa wakinuka pombe, naamini kila anayejijua mnywaji atakuwa na nidhamu ya barabarani kwa kuamua ama anywe pombe au aendeshe gari.

Dereva lazima afahamu kuwa uhai wake na abiria ni wa thamani, hivyo lazima kuheshimu sheria za barabarani ikiwa ni pamoja na kutoendesha gari huku ukiwa umelewa.

Haya yote ni kwa sababu madereva wengi wako barabarani lakini hawazifahamu kabisa kanuni, taratibu na sheria mbalimbali za barabarani na ndio maana wako wanaoendesha magari wakiwa wemekunywa pombe tena nyingi hadi kiasi cha kulewa na kuyumba kabisa.

Naamini katika kudhibiti ajali za barabarani zinazotokana na ulevi, pia abiria au watumiaji wengine wa vyombo vya moto wanapaswa kusimama kidete na kukemea madereva wanaokiuka taratibu na Sheria za barabarani kama hawa.

Mara nyingine ukikaa karibu tu ya dereva unasikia harufu ya pombe, lakini kwa sababu wewe abiria unataka kuwahi ‘unapotezea’ na matokeo yake mnasafiri mkiendesha na dereva mlevi, yakitokea ya kutokea ndipo unasikia mtu anasema tena alikuwa amelewa ananuka pombe.

Wananchi wote kwa pamoja tukiwa na msimamo wa pamoja na kuendesha kampeni kwa kushirikiana na askari wa Usalama Barabarni kukemea, kukataa ajali za barabarani kwa kuwakataa madereva wazembe, walevi na wasiothamini maisha ya watu hakika tunaweza kukomesha matukio haya.HABARILEOA
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: