BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RUZUKU, SHERIA KAA LA MOTO KWA VIONGOZI WANAOUNDA UKAWA, KUWAGAWA MWAKA 2015

5 Mwenyekiti wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba

MGAWANYO wa ruzuku na kikwazo cha Sheria ya Vyama vya Siasa, vinatarajiwa kugeuka kisu kikali, kitakachotishia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.

Tayari Ukawa imetangaza nia ya kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu, na mgombea udiwani, ubunge na urais mmoja katika uchaguzi mkuu ujao, utakaofanyika mwakani.

Mwenyekiti wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, alitoa tamko la mgombea mmoja jana mbele ya waandishi wa habari, ambapo alifafanua kuwa, mgombea huyo katika kila nafasi kuanzia kitongoji mpaka urais, atateuliwa kwa kufuata vigezo vitakavyokubaliwa na vyama hivyo.

Alisema uchaguzi huo wa serikali za mitaa, kwao ni nguzo muhimu ya kufikia malengo yao ya kushika dola na hatua hiyo itathibitisha kuwa Ukawa ni ushirikiano thabiti, ulioazimia kuwapa wananchi njia bora ya ukombozi.

Katika kudhihirisha nia hiyo, Profesa Lipumba alisema Oktoba 26 mwaka huu, wanatarajia kusaini makubaliano ya pamoja ya wanachama wa Ukawa, katika mkutano wa hadhara utakaofanyika jijini Dar es Salaam.

Sheria
Hata hivyo, tamko hilo la Profesa Lipumba, halikufafanua changamoto iliyotolewa hivi karibuni na aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, kwamba Ukawa hauwezi kuweka mgombea mmoja katika mazingira ya sasa ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Tendwa alitaka vyama hivyo kabla ya kufikia hatua hiyo, vipigie kampeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ambao aliuacha ofisini kwake kabla ya kustaafu, kwa kuwa unaruhusu wao kuungana na kuweka mgombea mmoja.

Kwa mujibu wa Tendwa, kwa sheria ya sasa ya vyama hivyo vinaweza kumuunga mkono mgombea wa chama fulani, lakini haviwezi kuwa na umoja utakaopewa jina, kisha kusimamisha mgombea mmoja huku kila chama kikibaki na utambulisho wake.

Tendwa ambaye alizungumza na gazeti moja la kila siku (si HabariLeo), kuhusu utata wa kuweka mgombea mmoja, alisisitiza kwamba Ukawa hawawezi kuutumia kusimamisha mgombea mmoja katika Uchaguzi Mkuu.

Alifafanua kuwa muungano huo wa Ukawa sio wa kisheria, hauwezi kuweka mgombea mmoja wa urais na kumuita mgombea wa Ukawa kwa kuwa sheria haisemi hivyo.

Ruzuku
Mbali na sheria, Tendwa pia alisema hata utaratibu huo ukianzishwa na vyama hivyo vikapata nguvu ya kisheria kuungana na hivyo kuweka mgombea mmoja, ni lazima upatikane ufumbuzi kuhusu ruzuku.

Kwa mujibu wa Tendwa vyama hivyo vitatakiwa kujiridhisha ruzuku itakwenda wapi, kama ni katika umoja au chama kupitia mbunge.

Alitoa mfano wa Kenya, ambako Sheria inaruhusu vyama kuungana na kuweka mgombea mmoja, ambako alisema wanachofanya ni asilimia fulani ya ruzuku kwenda katika umoja na inayobaki kuingia kwenye chama kupitia mbunge.

Upungufu uchaguzi
Pamoja na kutangaza nia ya kuweka mgombea mmoja katika uchaguzi wa serikali za mitaa bila kujali mazingira magumu ya kisheria yaliyopo, Profesa Lipumba pia alisema baada ya kupitia kanuni za uchaguzi huo, wamebaini upungufu mkubwa ambao wanahitaji kupata ufafanuzi wa kina.

Alitaja mambo ambayo alisema yana upungufu kuwa ni idadi ya siku za kuandikisha wapiga kura kutowekwa wazi kwenye kanuni, utata wa fomu za wagombea na karatasi ya wapiga kura inayohusu wao kutakiwa kujaza nembo ya chama na halmashauri.

Pia alihoji kwanini muda wa mwisho wa kampeni, umewekwa saa 11 jioni wakati kwa Sheria ya Vyama va Siasa inaweka wazi kuwa muda wa mikutano ya siasa ni saa 12 jioni.

Dk Slaa

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa alisema, kwa sasa wanajipanga kuhakikisha Katiba Inayopendekezwa inapingwa kwa nguvu zote, ambapo alisema watahakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili waikatae katiba hiyo popote walipo.

“Iwe ni vijiweni kwenye kahawa, mashambani, majumbani au kwingine kokote kule. Tutahakikisha haki za Watanzania zinadaiwa kwa nguvu zote na kile walichokileta wao (Katiba Inayopendekezwa), kinapingwa kwa nguvu zote,” alisema Slaa.

Hata hivyo,Ukawa watakabiliana na upande mwingine unaotoa elimu ya kuikubali Katiba hiyo, unaoungwa mkono na asasi za kiraia, Chama Cha Mapinduzi na hata Rais Jakaya Kikwete.

Kwa mfano, Rais Kikwete alipokuwa ziarani Mwanza hivi karibuni alisema; “Sijui Katiba nyingine duniani ambayo inajadili makundi yote ndani ya jamii kama hii Katiba Inayopendekezwa. “Hakuna aliyeachwa – wavuvi wamo, wajane wamo, wafanyabiashara ndogo wamo, akinamama lishe wamo, wakulima wamo, wafugaji wamo….kila mtu yumo.

Akinamama ndio usiseme kabisa wao wamepata hata asimilia 50 kwa 50 ndani ya Bunge. Aliongeza Rais Kikwete:“ Hivi Katiba mbaya inakuwa kama inayopendekezwa na kama hii inayopendekezwa ni mbaya sasa hivi nzuri ikoje?”HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: