BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI YAIBUA MADUDU NA KASHFA YA KUTISHA IKIWE ZAIDI YA SH1,00 BILIONI ZIKIYEYUKA.....!.


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akiwasilisha taarifa ya kamati yake katika kikao cha tatu cha Mkutano wa 18 wa Bunge, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi


Dar es Salaam.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeanika madudu na kashfa za kutisha katika ripoti maalumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikiwa ni pamoja na zaidi ya Sh100 bilioni kukwepwa kulipwa na kampuni mbalimbali kwa kivuli cha misamaha ya kodi.


Ripoti hiyo iliyowasilishwa jana na Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe imeeleza ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, jinsi ujenzi wa jengo la watu mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam (JNIA), ulivyofanyika bila kibali kutoka Baraza la Mawaziri, huku mchango wa ujenzi wa jengo hilo kwa Serikali ukiongezwa kwa Sh2.3 bilioni.


Pia, imeibua udanganyifu uliofanyika katika nyumba za Bodi ya Korosho na Bodi ya Sukari ambazo kwa sasa zinatumiwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Silvestry Koka.


Alisema hadi kufikia Juni 30, 2013 misamaha ya kodi iliyokuwa imetolewa ilikuwa Sh 1.5 trilioni lakini hadi Juni 2014, misamaha hiyo iliongezeka kwa asilimia 22.6 mpaka kufikia Sh 1.8 trilioni.


Zitto alisema: “Mwaka 2012/13, CAG alibaini ukiukwaji wa maelekezo ya Serikali uliosababisha hasara ya Sh22.3 bilioni kutokana na kuhamishwa kwa mafuta yenye msamaha wa kodi kutoka kwa kampuni za madini kwenda kwa makandarasi mbalimbali.”


Alisema Kampuni ya M/S Geita Gold Mines na Resolute Tanzania Limited zilihamisha mafuta yaliyosamehewa kodi yenye thamani ya Sh22.3 bilioni kwenda kwa makandarasi mbalimbali (M/S Geita Gold Mines, Sh22 bilioni na Resolute Tanzania Limited, Sh20 milioni).


Alisema uhamishaji huo ulikuwa ni kinyume na tangazo la Serikali la Oktoba 25, 2002 lililoelekeza kusitisha msamaha wa kodi pale ambako mafuta yaliyosamehewa kodi yatatumika kwa matumizi tofauti na yaliyokusudiwa au yatahamishiwa, kuuzwa au kupewa mtu mwingine ambaye hana haki ya kupewa msamaha huo.


Alisema matumizi ya misamaha ya kodi kwa malengo tofauti na yaliyokusudiwa pia yalisababisha upotevu wa mapato ya Sh392.7 milioni.


“Mwaka 2011/2012 na 2012/2013 Kampuni ya Kiliwarrior Expeditions Ltd ya Arusha iliagiza magari 28 na kusamehewa kodi yenye thamani ya Sh465 milioni, lakini ukaguzi maalumu umebaini kuwa kampuni hiyo inamiliki magari mawili tu ambayo si kati ya yale 28 yaliyoingizwa nchini kwa msamaha wa kodi,” alisema na kuongeza: “Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato (Arusha) ilikiri kuwa baadhi ya magari hayo yalisajiliwa na TRA na yanatumiwa na watu binafsi ambao hawakuwa na haki ya kupewa msamaha wa kodi.”


Alisema ripoti hiyo pia inaeleza jinsi misamaha ya kodi iliyotolewa kwa kampuni isiyostahili yenye thamani ya Sh53.3 milioni.


“Kampuni ya Kilemakyaro Mountain Lodge Limited ilipewa msamaha wa kodi kwa ajili ya mradi wa ujenzi na upanuzi wa hoteli kadhaa katika Kijiji cha Changarawe wilayani Karatu, Arusha. Ukaguzi Maalumu umebaini kuwa Kampuni hiyo iliagiza magari matatu kwa kutumia msamaha huo wa kodi na magari hayo yalipata msamaha wenye thamani ya Sh72.6 milioni.”


Inaeleza kuwa wakaguzi walipokwenda kukagua mradi huo, hawakukuta gari hata moja ingawa menejimenti ya kampuni ilithibitisha ununuzi wa gari moja tu na haikuwa na taarifa ya ununuzi wa hayo mengine.


Alisema utoaji wa misamaha ya kodi isiyo na ukomo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ukarabati na upanuzi wa kampuni mbalimbali uliikosesha Serikali mapato ya Sh63.2 bilioni. Alisema kiwango hicho kimeongezeka kutoka Sh34.2 bilioni kwa mwaka 2011/2012 hadi Sh63.2 bilioni kwa mwaka 2012/2013, ikiwa ni ongezeko la asilimia 84.81.


Alisema ripoti inaeleza kuwa ukomo wa muda, kiasi na aina ya vifaa vinavyopewa msamaha wa kodi umetengeneza mianya kwa baadhi ya wawekezaji kufaidika na misamaha ya kodi isiyo na ukomo.


“Ripoti pia imebaini misamaha ya kodi ya Sh13 bilioni iliyotolewa kwa kuzingatia maombi yasiyo na nyaraka za kutosha,” alisema Zitto.


Alisema nyaraka zilizokosekana ni pamoja na kibali za msamaha wa kodi kutoka Hazina, kibali kutoka Wizara ya Fedha, taarifa ya matumizi yanayoendelea ya misamaha ya kodi kibali cha ujenzi, taarifa za ukaguzi wa kushtukiza.


Uwanja wa ndege
Kuhusu ukaguzi maalumu wa ujenzi wa jengo la kumbi za watu mashuhuri JNIA katika kipindi cha 2006 hadi 2012 katika awamu ya kwanza, Zitto alisema CAG alibaini ukikuwaji wa taratibu katika miradi mitatu… “Ilibainika kuwa ujenzi kuanza kufanyika bila kupata kibali cha Baraza la Mawaziri.”


Alisema hati za makubaliano baina ya Wizara ya Miundombinu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na (TAA) na mkandarasi, China Songangol International Limited (CSIL), zilikuwa na upungufu na hazikuwa zimesainiwa na Waziri wa Miundombinu, hazikuwa na tarehe wala namba.


Alisema waraka huo haukuwa na uthibitisho iwapo Baraza la Mawaziri liliridhia kwa hatua zaidi za kumshauri Rais ili kuagiza ujenzi wa jengo hilo.


Zitto alisema kutokana na hali hiyo, PAC itahitaji kupata maelezo ya kina ya Serikali iwapo mchakato wa kuruhusu ujenzi wa jengo hilo ulipitia taratibu zote za kupata idhini ya Baraza la Mawaziri ikizingatiwa kuwa Kampuni ya CSIL baadaye ilishindwa kutekeleza majukumu yake ya kimkataba ikiwamo uendelezaji wa eneo la Terminal Three katika Uwanja wa JNIA.


Akizungumzia mkanganyiko kuhusu mchango wa Serikali katika ujenzi wa jengo hilo, Zitto alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa Serikali ilichangia kiasi cha Dola za Marekani milioni mbili (Sh3 bilioni).


“Ripoti inaeleza ukaguzi maalumu baada ya kupitia na kuchambua nyaraka mbalimbali za mikataba na ununuzi ilithibitisha kuwa gharama za mchango wa Serikali katika jengo la kumbi za watu mashuhuri kwa kazi zilizofanyika ulikuwa ni Sh869 milioni na siyo Sh3 bilioni. Serikali ijibu utata huu,” alisema.


Alisema katika ukaguzi huo maalumu, wakaguzi walishindwa kupata nyaraka wala vielelezo vyovyote vilivyomo kwenye majalada ya TAA na yale ya JNIA ikiwamo mkataba kwa ajili ya kuonyesha gharama halisi za ujenzi wa jengo hilo.


“Kukosekana kwa mikataba hiyo, kunaashiria kwa mkandarasi pamoja na mfadhili (M/s China International Fund Limited), hawakukabidhi nyaraka za ujenzi serikalini na hivyo kushindwa kufahamu gharama halisi iliyolipwa na mfadhili huyo,” alisema.


Alisema ripoti inaonyesha katika mikutano mbalimbali ya Bunge mwaka 2011 na 2012, Serikali ilitoa tamko kuwa jengo la watu mashuhuri lilijengwa kwa Sh12 bilioni, tofauti ya Sh9 bilioni kutoka gharama iliyoainishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali.


Zitto alisema kulikuwa na ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi kulikofanywa na TAA na kwamba ununuzi wa jumla ya Sh916 milioni uliofanywa mamlaka hiyo ulikuwa kinyume na sheria hiyo.


Sakata la Wasira na Koka
Kuhusu nyumba ya Bodi ya Sukari ambayo kwa sasa anaishi Waziri Stephen Wasira, ripoti hiyo imeeleza kuwa nyumba hiyo haijarudishwa kwenye umiliki wa bodi tangu Februari 12, 2008 kiongozi huyo alipoteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Uratibu na Uhusiano.


Zitto alisema licha ya Katibu Mkuu Kiongozi kuahidi kuwa nyumba hiyo ingerudishwa tangu Desemba, 2011 mpaka kamati hiyo inawasilisha taarifa hiyo nyumba hiyo ilikuwa haijarudishwa.


PAC imeitaka Bodi ya Sukari kumwandikia barua ili arudishe nyumba hiyo na Msajili wa Hazina kuhakikisha umiliki wa nyumba hiyo unabaki kwa Bodi ya Sukari.


Pia, PAC ilieleza jinsi ripoti ya CAG ilivyoeleza hati ya nyumba ya Taasisi ya Kilimo Tanzania ilivyofutwa mwaka 1963, kabla ya mtu mwingine kuibadilisha mwaka 2011 na kuiuza kwa Koka.


“Kamati imepata taarifa kutoka kwa CAG kuwa Bodi ya Korosho ilinyang’anywa umiliki wa nyumba hiyo iliyopo eneo la Ursino, Upanga Dar es Salaam. Baada ya hati kubadilishwa, Mamlaka ya Korosho iliwasilisha nyaraka za zuio ili kuzuia muamala wowote kuhusu miliki hiyo usifanyike.”


Aliongeza: “Muamala uliofanyika una mazingira ya udanganyifu, kamati inapenda kusisitiza uchunguzi wa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), ukamilike haraka iwezekanavyo ili wahusika wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.”


TPA


Kamati imebaini kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imefanya ununuzi wa dharura unaofikia Sh8 bilioni bila kupata kibali kutoka kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali.


Kusuasua TTCL
Kusuasua kiutendaji kwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kukosekana kwa wawekezaji kumesababisha kampuni hiyo kuwa na mtaji hasi wa Sh87.8 bilioni, sambamba na kupata hasara ya takriban Sh334 bilioni mpaka kufikia mwaka 2013.


Zitto alisema katika miaka miwili, kampuni hiyo imepata hasara ya Sh36 bilioni. TTCL ilianzishwa baada ya kuvunjwa kwa lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania mwaka 1993. Hivi sasa hisa za TTCL zinamilikiwa na Serikali na Kampuni ya Bharti Airtel Tanzania B.V kwa uwiano wa asilimia 65 na asilimia 35.


“Kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa, TTCL ilipata hasara ya Sh20.8 bilioni mwaka 2012, Sh16.2 bilioni mwaka 2013. Mpaka kufikia mwaka 2013, kampuni ilikuwa imepata hasara ya Sh334.48 bilioni,” alisema.


Alisema ukubwa wa hasara hiyo umeiondolea TTCL mvuto wa kukopeshwa na taasisi za fedha hata zile zenye nia ya kufanya hivyo.


Alisema: “Tangu TTCL ibinafsishwe mwaka 2001, hakuna uwekezaji mkubwa uliofanyika na mpango wa kutafuta mkopo kutoka benki za ndani na nje ya nchi unakwamishwa na masharti ya kupata udhamini wa Serikali.”


Alisema mwaka 2005, Serikali iliipa TTCL mkopo wa Dola 28 milioni za Marekani milioni 28 kwa ajili ya kulipa wafanyakazi waliostaafishwa, lakini deni hilo halijalipwa mpaka sasa na umefikia Sh76.6 bilioni pamoja na riba.


“Mbali na deni hilo, TTCL inadaiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Sh25 bilioni hivyo kufanya jumla ya deni kuwa Sh101.6 bilioni,” alisema.


Alisema Serikali inatakiwa kufanya uamuzi wa haraka kuikwamua kampuni hiyo ili iweze kuendelea kutoa huduma kwenye sekta ya mawasiliano nchini.


Katika ripoti hiyo, pia imeelezwa deni la Sh1.8 trilioni ambalo Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi za jamii.


Deni hilo ni mbali na deni la Sh7 trilioni ambalo Serikali inadaiwa na Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF) ambalo lilianza mwaka 1999 baada ya PSPF kulipa mafao ya wanachama ambao kisheria walistahili kulipwa lakini walikuwa hawachangii kwenye mfuko huo.


Gharama za machapisho
Aidha, ukaguzi maalumu uliofanywa na CAG umebaini kuwa Serikali imetumia Sh2.5 bilioni katika kipindi cha miaka miwili kugharimia machapisho ya hotuba za bajeti za wizara 21 na taasisi tano katika magazeti.


Kati ya kiasi hicho, Sh184 milioni zilikuwa bado hazijalipwa hadi wakati wa ukaguzi huo wa mwaka 2013. Machapisho ya hotuba za bajeti yalifanyika mwaka 2011/12 na 2012/13.


Zitto alisema kwamba, Wizara ya Nishati na Madini pekee kwa mwaka wa fedha 2012/13 ilitumia Sh211.5 milioni kwa ajili ya kutangaza hotuba ya bajeti yake.


“Chombo cha habari kiitwacho Jambo Concepts Tanzania kililipwa Sh49.01 milioni ndani ya siku moja kwa ajili ya kutangaza Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo Juni 13, 2013,” alisema. “Jambo la kujiuliza ni msingi upi wizara iliutumia katika kulipia kiasi kikubwa cha fedha kwa chombo cha habari kimoja kwa tangazo la siku moja wakati kwa vyombo vingine vya habari vililipwa wastani wa Sh9 hadi 11 milioni kwa huduma ya aina hiyo?”


Zitto alisema huo ni ushahidi wa wazi kuwa kumekuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma yenye taswira za upendeleo kwa baadhi ya taasisi.


Alisema hali hiyo inazifanya taasisi hizo kutumia mwanya wa kutangaza hotuba za bajeti za wizara kwa malengo yasiyo bayana na ni viashiria vya matumizi mabaya ya madaraka na kukosekana udhibiti wa matumizi ya fedha.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: