BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CCM YAPULIZA FILIMBI KWA KUTANGAZA KUANZA KAMPENI ZA KUWANIA KUTEULIWA KUGOMBEA URASI 2015.


Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, David Mathayo wakishiriki ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari ya Kata ya Njoro wakati wa ziara yake jimboni humo juzi. Picha na Adam Mzee.

FILIMBI kwa ajili ya kuanza kampeni za kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi za udiwani, ubunge na urais, itapulizwa rasmi Juni mwaka huu.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimesema kitasikiliza sauti ya wengi katika kumteua mgombea wa urais, wabunge na madiwani katika Uchaguzi Mkuu ujao, ilimradi mgombea atakayepaziwa sauti na wengi awe na sifa stahili.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema hayo jana alipozungumza na wajumbe wa halmashauri ya Jimbo la Same Magharibi akiwa ziarani wilayani humo kushiriki na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Katibu Mkuu huyo wa CCM alisema kutokana na ratiba hiyo, hakuna ruhusa kwa mwanaCCM yeyote kuanza kampeni kabla ya muda huo, kwa vile hatua hiyo itatibua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa kipindi cha uongozi kilichosalia.

“Tuwaache madiwani na wabunge waendelee kufanya kazi zao. Madiwani na wabunge wengi wanafanya kazi nzuri, ndio maana tunaona miradi mingi inatekelezwa, tukianza kampeni tutawachanganya na hawatafanya kazi zao kikamilifu,” alisema Kinana.

Akizungumzia uteuzi kwa wagombea, Kinana alisema chama hicho kitazingatia maoni ya wanaCCM wengi katika kumpata mgombea ili kutoa haki kwa vile chama hicho kimekuwa kikipoteza uongozi katika baadhi ya maeneo kutokana na kutotenda haki.

“Hili suala la haki si tu kwamba linasemwa kwa ngazi ya chini, hata sisi tulio katika ngazi ya juu tunapaswa kuzingatia hili. Sio wanachama wengi wanasema hivi halafu sisi tunamleta mgombea mwingine, yaani tunapingana na wapiga kura ambao ni wengi. “Mgombea atakayekubalika na wengi ndiye atakayepitishwa ili mradi tu awe na sifa zinazostahili,” alisema Katibu Mkuu huyo wa CCM.

Alishauri wanachama na wananchi wa Jimbo la Same Magharibi, kuwachagua tena madiwani na Mbunge, Dk Mathayo David Mathayo, kutokana na kazi kubwa waliyoifanya ingawa alisisitiza kuwa hiyo haiondoi haki kwa wanaCCM wengine kujitokeza kugombea.

“Unajua kuna haki lakini pia kuna busara katika kuchagua viongozi. Haki ni kwa mwanaCCM yeyote kujitokeza kugombea, lakini wakati mwingine busara inatumika kupima kile alichofanya kiongozi aliyepo madarakani katika kuwaletea maendeleo, na hivyo kustahili kuchaguliwa tena,” alisema Kinana.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: