BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MISWADA MIWILIYA SHERIA ZA HABARI YAONDOLEWA BUNGENI DODOMA.



MISWADA miwili ya sheria inayohusu sekta ya habari iliyokuwa iwasilishwe katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini hapa chini ya hati ya dharura, imeondolewa.

Ratiba mpya iliyotolewa na ofisi ya Bunge mjini hapa jana, imeonesha kuwa miswada hiyo; wa Sheria ya Kupata Habari wa Mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari, haimo katika shughuli za kikao cha Bunge hili.

Miswada hiyo katika ratiba ya awali ilionesha ilikuwa iwasilishwe jana Ijumaa; lakini baadaye ofisi ya Bunge ilitoa ratiba nyingine ambayo ilionesha kuwa miswada hiyo imesogezwa mbele na ingewasilishwa Jumanne wiki ijayo.

Ratiba ya tatu iliyotolewa jana na Bunge, ilionesha kuwa shughuli zilizobaki katika kikao cha 10 cha Bunge, miswada hiyo haimo.

Hatua hiyo inatokana na kikao cha Kamati ya Uongozi kilichofanyika juzi jioni, kuamua kusikiliza kilio cha wadau wa sekta ya habari ambao wamekuwa mjini hapa kuhakikisha hati ya dharura inaondolewa katika miswada hiyo.

Tangu miswada hiyo ya sheria iingizwe kwenye shughuli za ratiba ya mkutano wa 19 wa Bunge ambao ulianza Machi 17, wadau mbalimbali wa habari walijitokeza kupinga hatua hiyo ya Serikali, kwa maelezo kwamba kuna usiri mkubwa uliotokana na wadau wa sekta ya habari kutopewa fursa ya kutoa maoni yao.

Wadau waliiandikia Ofisi ya Spika, Anne Makinda na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakiomba miswada hiyo isiwalishwe kwa hati ya dharura, badala yake ifuate taratibu zake zote ili kutoa fursa kwa wadau kutoa maoni yao.

Kwa muda wa wiki sasa, wadau wa habari wamekuwa mjini hapa wakifanya vikao mbalimbali na wabunge pamoja na maofisa wa Serikali, kuwaeleza umuhimu wa miswada hiyo kujulikana kwa wadau na hatimaye watoe maoni yao.

Wadau wa sekta ya habari wamekuwa wakiishutumu Serikali kuwa licha ya kuiwasilisha chini ya hati ya dharura, lakini pia kumekuwa na usiri mkubwa juu ya kilichomo kwenye miswada hiyo, kutokana na wadau wenyewe kutopewa hata nakala ili wapate muda wa kuipitia.

Katika siku za mwanzo za mkutano wa Bunge unaoendelea mjini hapa, Mbunge wa Kisarawe Selemani Jaffo (CCM), alihoji bungeni sababu ya miswada hiyo kuletwa kwa hati ya dharura wakati kuna malalamiko ya wadau wa habari kuwa hawakushirikishwa.

Hata hivyo, Spika Anne Makinda aliliambia Bunge kuwa hajapata hati ya dharura kutoka serikalini kama inavyoelezwa juu ya miswada hiyo, jambo ambalo liliendelea kuweka wingu kuhusu uwasilishwaji wake bungeni.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo mpya ya Bunge, jana Bunge lilijadili Muswada wa Sheria wa Bajeti wa Mwaka 2014, ambayo mjadala wake utaendelea hadi leo na muswada wa sheria wa Baraza la Vijana wa mwaka 2015 utawasilishwa bungeni.

Siku ya Jumatatu Muswada wa Sheria wa Wataalamu wa Mambo ya Kemia na Muswada wa Sheria wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, itawasilishwa bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu.

Ratiba inaonesha kuwa siku ya Jumanne ambako ilikuwa imepangwa miswada wa sekta ya habari kuwasilishwa, sasa siku hiyo, Muswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki wa mwaka 2014 na wa Makosa ya Mtandao, itawasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza na hatua zake zote chini ya hati ya dharura itajadiliwa bungeni na kupitishwa siku hiyo.

Siku ya Jumatano ambayo bunge litaahirishwa, muswada wa sheria mbalimbali ikiwemo masuala ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi itajadiliwa na baadaye Waziri Mkuu atatoa hoja ya kuahirisha Bunge.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: