BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NCHI NZURI KAMA TANZANIA, KWELI TUWAPE MATAPELI ?.

http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2013/11/mtatiro.jpg
Tanzania ni nchi nzuri sana, nchi iliyowakuza babu zetu na kizazi kilichopita, nchi iliyowalea wazee wetu na watu muhimu kwetu, nchi iliyowaleta mama zetu na kufanikisha malezi yetu katika amani ya kudumu, nchi hii ni nzuri sana na haiwezi kukabidhiwa kwa watu wenye nia ovu.


Kwa nini uwe na kitu chenye muhimu kama lulu, kizuri kama dhahabu na cha thamani kama almasi kisha ukakitoa na kukitupa jalalani? Tanzania ni lulu yetu, ni dhahabu yetu na ni almasi yetu – kamwe hatuwezi kuitupa jalalani.


Hivi sasa majalala yamejaa kila kona, matapeli wamejaa kila tuendako na wanatumia kila mbinu iwayo kupewa nchi hii nzuri.


Nimekaa na kutafakari na kujiuliza ni Mtanzania gani mwenye dhamira ya dhati anataka kuitupa lulu yake na dhahabu yake jalalani? Ni nani anataka kuigawa nchi hii tamu kwa matapeli na watu wasio na aibu? Naamini hakuna mtu huyo na kama yupo ana matatizo yake.


Huu ni mwaka wa uchaguzi na kuna watu watakuwa wanahangaika huku na kule kwa waganga kutafuta dawa za kuwalewesha wapiga kura, ati wakitamka “wataleta maji” wapiga kura wayaone yanatiririka na kuanza kuwapigia kura, wanatafuta mazingaombwe na uchawi ili wafanikiwe katika safari ya kisiasa na zaidi ya yote waongoze nchi nzuri kama Tanzania.


Je, tumejiandaa kuwakabidhi watu hao nchi nzuri kama hii, kwamba tunaikabidhi kwao ili iendeshwe kiganga, kwa ramli na kwa kutegemea maajabu! Viongozi wa namna hii wamejazana kila mahali na sisi wapigakura tunaishi nao na tunawajua sana.


Tunamjua nani anatafuta ubunge au udiwani na ama urais na kila kukicha amepaki gari lake kwa mpiga ramli fulani akiomba miungu imsaidie awapumbaze wapiga kura waliomchoka ili apate madaraka! Kweli nchi nzuri kama hii tutaikabidhi kwa watu hawa?


Kuna wengine tunawajua, wanakesha uchawini wakisaka viungo vya wenzetu wenye ulemavu wa ngozi “albino” na viungo vya watoto wachanga. Wengine wanatumwa baharini usiku wa manane kwenda kujiganga na kutafuta bahati, wanahangaika na kusaka uongozi wa damu, hawana shida kufanya lolote lile, kuua, kukatili, kutweza na kutesa ilimradi wawe viongozi Oktoba.


Hawa nao tunawajua vizuri na hasa wanakoishi na wanakotoka na wanayoyafanya, nilikuwa tu najiuliza kwamba na hawa tunawapa nchi nzuri kama Tanzania? Wauaji, watu katili wasio na soni wala chembe ya huruma, wanaotumia damu ili kupata nchi yetu, lulu yetu – hawa nao tutawakabidhi nchi nzuri kama Tanzania? Nauliza tu?


Huu ni mwaka wa uchaguzi na kuna wale wanaojipitisha na kutoa ahadi za upendeleo kwa watu watakaowaunga mkono, “wewe nitakupa ubunge- nisaidie, wewe nitakupa ukurugenzi nipigie kampeni, wewe nitakupa ukuu wa mkoa nipiganie, wewe nitakupa cheo kikubwa jeshini nipiganie, wewe ntakupa safari nyingi za nje nipambanie, wewe hutalipa ushuru ukiingiza bidhaa nitetee, wewe mumeo atatolewa gerezani nikiingia madarakani nililie, wewe mwanao atasoma Uingereza kwa gharama za serikali nipe nafuu….”.


Nchi nzuri kama hii inagawanywa vipande vipande kabla ya Oktoba, wajanja wanagawana nafasi zote ambazo zingepewa kwa watu weledi, na wanaozigawa tunawajua, wanajipitisha huku na kule wakizigawa, najiuliza hivi tumejiandaa kuigawa nchi nzuri kama hii kwa watu hawa? Watu wanaoamini kuwa wanaweza kuiuza nchi yetu kwa kugawa vyeo, ardhi, kodi zetu n.k. Nchi nzuri kama Tanzania!


Kuna wale wenzangu na mimi ambao tuliwapatia fursa miaka mitano iliyopita, wakawa viongozi kipindi chote hicho, mvua ilipotunyeshea nje hawakuja kutusaidia, jua lilipotuwakia hawakuwepo, mazao yalipotufia waliangalia kwa macho wakiwa mbali nasi.


Maji yalipotuishia wakasema tusubiri maajabu ya Mungu, magonjwa yalipotunyemelea walituambia madaktari hakuna na vitisho vilipotujia walituambia tupambane kivyetu. Lakini hawa si walikuwa wawakilishi wetu tuliowachagua kwa kura zetu na mapenzi yetu? Tulipowachagua wakatugeuka kiasi hicho, wakatukimbia, wakajenga na kuishi mijini wakatuacha huku vijijini?


Leo tarehe zimekaribia, imebaki miezi michache wanajipitisha wakiwa na kanga, wakiwa na Vicoba, wakiwa na miradi ya vijana, wazee na wanawake, wakihudhuria misiba yetu na kutuuliza habari za asubuhi mara kumi kumi.


Matapeli wakubwa hawa na wao bado tuna nia ya kuwakabidhi nchi nzuri kama hii? Tuwape Tanzania yetu yenye neema walizoshindwa kuzifanyia kazi miaka minne iliyopita? Tukanyeshewa na mvua peke yetu, tukapigwa na jua peke yetu, tukasaka maji kilomita 20 peke yetu, tukajilinda wenyewe na tukajitibu wenyewe.


Wajanja hawa tuwape uongozi mara nyingine? Kwamba tuko tayari waendelee kuiharibu lulu yetu, nchi nzuri kama Tanzania! Najiuliza nani yuko tayari kuona nchi muhimu kama hii inaharibiwa na watu walewale walioshindwa tulipowapa nafasi?


Tukutane Jumapili ijayo.

(Julius Mtatiro ni kiongozi mzoefu, ana shahada ya uzamili (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB): +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com).
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: