BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VIJIJI VITATU VYAKUMBWA NA MAFURIKO KAHAMA, WATU 38 WAPOTEZA MAISHA NA KUJERUHI WENGINE 82.

 
Wakazi wa Kahama mkoani Shinyanga wakipita kwenye eneo lililofurika maji kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo iliyonyesha mkoani humo juzi.

MAAFA makubwa yameikumba Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga baada ya watu 38 kufa papo hapo na wengine 82 kujeruhiwa, kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali, iliyonyesha katika Kijiji cha Mwakata Kata ya Isaka.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema jana kuwa tukio hilo halijawahi kutokea mkoani humo. Baadhi ya majeruhi, akiwemo Paulina Malongo aliyefiwa na wajukuu wanne, walieleza hali ilivyokuwa.

Shughuli za uokoaji ziliendelea hadi jana chini ya Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alisema huenda idadi ya waliokufa na majeruhi, ikaongezeka.

Kamanda alisema mvua hiyo iliyosababisha maafa, ilinyesha juzi saa 3 usiku katika kijiji hicho ikiambatana na upepo mkali ulioangusha miti, kubomoa na kuezua nyumba, hivyo kusababisha vifo na majeruhi hao.

Inadaiwa wengi waliopoteza maisha ni watoto. Afiwa wajukuu wanne Baadhi ya majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama, walisema mvua ilikuwa kubwa ikiambatana na upepo mkali. Walisema nyumba ziliezuliwa na wakati huo huo upepo uling’oa miti.

“Tulikuwa tumelala majira ya saa tatu usiku ghafla tulisikia upepo mkali ukiambatana na mvua kubwa ya mawe. Maji mengi yaliingia ndani na ghafla nyumba yangu ilianguka na nimepoteza wajukuu wangu wanne,” alisema Paulina Malongo, ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho cha Mwakata.

Uokozi Kamanda Kamugisha alisema majeruhi walikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa ajili ya kupatiwa matibabu wakati jitihada zaidi za uokozi zikiendelea katika kijiji hicho.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk Joseph Ngowi akizungumza na waandishi wa habari, alisema amepokea majeruhi zaidi ya 60 na kati yao watatu walifariki wakati wakiendelea na matibabu hospitalini hapo.

“Hatuna idadi kamili ya watu waliojeruhiwa au waliokufa na tumetuma madaktari wetu kwenda katika kijiji hicho kwa ajili ya huduma ya kwanza pamoja na kufanya uchunguzi ili kubaini idadi kamili ya waliokufa,” alisema Ngowi.

Dk Ngowi alisema kutokana na umbali uliopo kutoka eneo la tukio hadi hospitali ya wilaya, wamelazimika kutuma jopo la madaktari kwenda eneo hilo, kubaini waliokufa na kuidhinisha maziko kupunguza gharama kwa wananchi waliofiwa.

Tathimini Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ilitegemea kukaa jana mchana kutathimini takwimu za uharibifu wa mali na idadi ya nyumba zilizokumbwa na maafa.

Mpesya alisema Jeshi la Zima moto na Uokoaji kwa kushirikiana na wananchi, wanaendelea na shughuli za uokoaji na huenda idadi ya waliokufa pamoja na majeruhi ikaongezeka katika tukio hilo. Watu wapatao 3,500 wameathiriwa na maafa hayo katika Kata ya Mwakata.

Kwa upande wa kaya zilizoathirika, 350 ni za Kijiji cha Makata, 100 za Kijiji cha Ngumbi na kaya 50 za Kijiji cha Magung’hwa. Athari zilizobainika papo hapo ni nyumba kadhaa, kuezuliwa na nyingine kubomoka, hali ambayo imesababisha kaya husika kukosa mahali pa kuishi. Aidha chakula cha akiba katika kaya hizo, kimeharibika na kingine kusombwa na maji.

Kikwete aomboleza Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Rufunga kuomboleza vifo vya watu 38 waliokufa na majeruhi zaidi ya 82.

“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 38 waliopoteza maisha na wengine 82 waliojeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa matibabu baada ya nyumba zao kusombwa kabisa na maji kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali kunyesha,” alisema Kikwete.

Katika taarifa iliyotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, Rais Kikwete amesema msiba huo siyo wa wana-Shinyanga pekee, bali ni wa taifa zima ambalo limepoteza nguvukazi muhimu kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii ya Watanzania kwa ujumla.

“Naomba upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kupotelewa ghafla na wananchi 38 kwa mara moja katika Mkoa wako.

Kupitia kwako, naomba rambirambi zangu na pole nyingi ziwafikie wafiwa wote kwa kuondokewa na wapendwa, ndugu na jamaa zao,” alisema.

Rais Kikwete aliwaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira wakati huu wa majonzi makubwa kwao wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao. Aliwataka kutosahau ukweli kwamba kazi ya Mungu haina makosa.

Aidha, amewahakikishia wafiwa wote kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha kuomboleza msiba huu mkubwa kwao na kwa taifa.

“Namwomba Mola awawezeshe majeruhi wote wa tukio hilo wapone haraka ili waweze kuungana tena na familia, ndugu na jamaa zao na kuendelea na maisha yao kama kawaida”, alisema katika salamu zake za rambirambi.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: