BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CHAMA CHA WANANCHI (CUF) NA CCM WAANZA KUTIFUANA NA KUSHIKANA UCHAWI VISIWANI ZANZIBAR.


Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.

Homa ya kisiasa ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu imeanza kupanda Zanzibar, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza kulumbana kuhusu ugawaji wa majimbo.


Kazi ya ugawaji wa majimbo hayo ambayo ipo chini ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) imekuwa ikifanyika kabla ya uchaguzi mkuu na kuchukuliwa kama mtaji kwa kila chama kwa ajili ya kupata ushindi.

CUF kimeitupia lawama Zec kwa kuchelewa kutangaza mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi mkuu kwa madai kuwa CCM wamezuia kutangazwa kwa uamuzi wa Tume kutokana na kutoridhika na utaratibu uliotumika kuyagawa majimbo hayo.

Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (Cuf), Ismail Jussa Ladhu, akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapa kwenye viwanja vya Alabama juzi, alisema Zec inachelewa kutangaza majimbo mapya kwa sababu CCM hawajaridhika na uamuzi wa tume hiyo.

Alisema kwa muda mrefu, Zec imekuwa ikiahidi kutoa matokeo ya ugawaji wa majimbo mapya kwa Unguja na Pemba, lakini imeendelea kukaa kimya huku tetesi zikisema kuwa imeshamaliza kazi, isipokuwa CCM haijaridhishwa na uamuzi huo.

Hata hivyo, Jussa hakueleza uamuzi wa Zec kuhusu ugawaji huo kama kuna mapya au kuna yaliyounganishwa.

“CCM imepatwa na degedege kuhusu ugawaji wa majimbo na ndiyo maana mpaka sasa uamuzi wa Tume ya Uchaguzi umekaliwa, tunaiambia kuwa endapo matokeo hayo watayachakachua kwa kufuata matakwa ya CCM hatutakubali, tutakula sahani moja mwaka huu,” alisema Jussa.

KAULI YA CCM
Akijibu tuhuma hizo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema CUF wana akili ndogo ya kufikiri na kwamba wameshachanganyikiwa kutokana na homa ya joto la uchaguzi mkuu.

Vuai alisema CCM inaongozwa kwa mujibu wa sheria na katiba, hivyo aliwaonya kuacha kukipakazia maovu chama hicho.

Alisema CUF wamechanganyikiwa na wana matatizo makubwa katika kuwapata wagombea kwenye majimbo na hawajui nani wamuweke katika majimbo ya uchaguzi.

“CUF kina matatizo makubwa, kama hawana imani na Tume ya Uchaguzi wakati tume hiyo inaundwa na wajumbe wakiwamo kutoka CUF, basi waipeleke mahakamani, lakini siyo kuipaka matope CCM,” alisema.

Vuai alisema kuwa CUF wana tamaa ya kuongezwa majimbo Unguja, lakini hawakubaliani na suala la kupunguzwa majimbo Pemba kutokana na idadi ndogo ya watu katika majimbo hayo.

MAJIBU YA ZEC
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Zec, Salum Ali Kassim, alisema tume hiyo haijamaliza kazi ya kuamua mgawanyo wa majimbo kama wanavyodai CUF.

“Nikwambie ndugu mwandishi, muulize huyo Jussa je; anaweza kuthibitisha kama ni kweli Tume imemaliza kazi na habari hizo kaambiwa na nani au kazipata kutoka kwa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ambao wanatoka CUF?” alihoji Mkurugenzi huyo.
Kassim alieleza kuwa wiki hii wanatarajia kufanya kikao na waandishi wa habari kuwaeleza tume hiyo ilipofikia kuhusiana na suala hilo la ugawaji wa majimbo.

Zec ilifanya mapitio ya ugawaji wa majimbo mwaka 2005 na kupunguza majimbo ya Pemba kutoka 21 hadi 18 wakati Unguja yaliongezwa kutoka 29 hadi 32. CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: