BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VYAMA VINAVYOUNDA UMOJA WA KATIBA YA WANANCHI (UKAWA) WAANZA KUGAWANA NCHI YA TANZANIA.

https://hivisasa.co.tz/wp-content/uploads/2014/04/ukwaaa.jpg
Viongozi wa Ukawa

Dar/Mikoani.
Katika kile kinachoonekana kuendelea kujiimarisha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimegawana maeneo mbalimbali nchini vikifanya mikutano ya hadhara na mafunzo kwa viongozi wake ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa ushindi.


Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.
Chadema kilianza ziara zake mikoani wiki zilizopita baada ya kuzindua mkakati wake uitwao ‘Hakuna kulala, Hakuna kula, Mpaka Kieleweke’ nchi nzima wakati timu ya NCCR-Mageuzi ikiweka kambi mkoani Kigoma kwa kile ilichokiita kuimarisha majimbo ya kimkakati.


Sanjari na vyama hivyo, CUF tangu juzi kiliingia katika moja ya ngome zake, mkoani Mtwara pamoja na mipango mengine ya kiushindi, kinahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura.


Jitihada za Ukawa kuzunguka mikoani zinakuja ikiwa ni majuma kadhaa tangu Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiongozwa na Katibu Mkuu wake Abdulrahman Kinana kilipomaliza ziara ya kujiimarisha na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010.


Pia, ziara hizo ziligongana na zile za Chama cha ACT - Wazalendo zilizosababisha Chadema na chama hicho kipya kugongana Butiama.


ACT - Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe kilihitimisha ziara yake ya kimkakati katika mikoa tisa inayoonekana kuwa ngome ya CCM, wiki iliyopita wilayani Bariadi, Shinyanga na kuvuna wanachama zaidi 6,000 katika mikoa hiyo.


NCCR-Mageuzi ipo Kigoma
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema jana kuwa Ukawa ina mikakati inayofanana ndani ya vyama vyao ya kuhakikisha inajiimarisha kisiasa nchi nzima ili ishinde Uchaguzi Mkuu.


Alisema siku 10 zilizopita, timu ya NCCR ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti - Zanzibar, Haji Hamis Hamad ilianza ziara Kigoma kuhakikisha majimbo ya mkoa huo yanaendelea kuwa ngome yake.


“Kigoma nzima ina majimbo yetu ya kimkakati na Ukawa wameshatukabidhi sasa kilichobaki ni kufanya ‘political management’ (usimamizi wa kisiasa) katika kiwango kinachotakiwa.


“Katika kikosi hicho, pia wamo Katibu Mwenezi, David Kafulila, Katibu Mkuu Mstaafu, Samuel Ruhuza na Kamishna wa Kagera, Peterson Mshenyela na wengineo,” alisema Nyambabe.


Alisema baada ya kumalizika ziara katika mkoa huo viongozi hao wataelekea Kagera kwa kuanzia majimbo ya Ngara na Nkenge, maeneo ambayo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anaendelea kumwaga ‘cheche’.


Kinachoendelea katika ziara hizo ni kama mashambulizi ya ‘bandika bandua’ na kuzuia mparaganyiko ndani ya vyama hivyo ambao unaweza kutokea baada ya kuanza kwa mchakato wa kugawana nafasi za udiwani na ubunge.


Chadema kila kona
Chadema, inayoendelea na utoaji wa mafunzo ya uongozi bora kwa viongozi wa ngazi zote na makada waliotia nia ya kugombea na mikakati mingine ya ushindi, viongozi wake wa juu wametawanyika maeneo tafauti katika kanda zake 10 za kiutendaji.


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa aliyekuwa Morogoro alieleza kuwa Tanzania kwa sasa inasifika nje ya nchi kwa uvunjifu wa haki za binadamu.


Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro juzi, Dk Slaa alisema katika kipindi cha miaka mitano, utawala wa Rais Jakaya Kikwete umekuwa na matukio mengi ya uvunjaji wa haki za binadamu.


Alisema hivi karibuni alikuwa Marekani kwa ziara maalumu na huko alihojiwa na waandishi wa habari katika kituo kimoja cha redio juu ya masuala ya utawala bora nchini.


Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu akiwa mkoani Rukwa alisema CCM imepoteza baraka za Mungu kiasi cha kushindwa kujua mgombea wake wa urais mpaka sasa, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya chama hicho.


Mwalimu aliyekuwa akizungumza kwenye Ukumbi wa Libori Mjini Sumbawanga, alisema viongozi wanaotokana na Chadema wapaswa kuwa tayari kusimamia haki kwa gharama zozote, kukataa rushwa na kupunguza kero kwa wananchi na kuwaonya wasije wakaufanya utawala wa Chadema kuwa kama wa CCM ambayo inayumba.


“Tuna miezi mitatu imesalia tuanze kampeni, lakini mpaka sasa CCM haijamjua mgombea wake, lini imewahi kutokea? Mungu amewachanganya kama wajenzi wa karavati,” alisema Mwalimu ambaye baada ya mkutano huo aliendelea na ziara yake mjini Makambako, Njombe.


Mwalimu alionyesha kushangazwa na baadhi ya wafuasi wa Chadema kujiunga na chama cha ACT – Wazalendo na akakiita kuwa ni chama cha msimu ambacho kitapotea baada ya Uchaguzi Mkuu.


Akiendelea na ziara yake mkoani Kagera, Mbowe alisema kusuasua kwa uandikishaji wa wapigakura ni kiashiria cha uvunjifu wa amani inayotokana na hofu ya CCM kuangushwa Oktoba.


Akiwahutubia wakazi wa Mji wa Bukoba juzi katika Uwanja wa Uhuru, Mbowe alisema nchi inaweza kuingia katika machafuko endapo litakuwapo jaribio lolote la kuahirisha Uchaguzi Mkuu kama upigaji kura wa Katiba Inayopendekezwa ulivyoahirishwa.


Alisema uchaguzi siyo suala la dharura na kila hatua inatakiwa kuwekwa wazi ili kuondoa hofu iliyoanza kujengeka kutokana na kubakia miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu.


Profesa Lipumba, Mtwara
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa endapo Wapinzani wataingia madarakani, kazi ya kwanza itakayofanyika ni kufumua mikataba yote iliyoingiwa bila kufuata taratibu.


Alisema asilimia kubwa ya mikataba iliyoingiwa na Serikali, haiwanufaishi Watanzania walio wengi na zaidi ya hapo haina tija kwa Taifa.


“Haiwezekani Watanzania wakaishi katika hali ya umaskini wakati wana rasilimali nzuri, zinazowafanya wafaidi matunda ya nchi yao, lakini kuna wajanja wachache wanaingia mikataba isiyo na tija, sasa tukiingia madarakani, tutaifumua,” alisema Profesa Lipumba ambaye leo atakuwa Kijiji cha Msimbati.


Juzi, akiwa katika Mji wa Mikindani mkoani Mtwara aliionya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuacha kushughulikia suala la Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na badala yake ijikite kuandaa mazingira ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ili kulinusuru Taifa kuingia katika mgogoro usio wa lazima.


Profesa Lipumba alisema NEC isipoteze rasilimali za Taifa na muda kwa jambo lisilo na tija kwa wakati huu.


“Jaji Lubuva (Damian, Mwenyekiti wa NEC) asiliingize Taifa katika mgogoro, ana haraka gani na Katiba Inayopendekezwa wakati hili la uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura hajalimaliza...? Ashughulikie hili la daftari ndiyo kazi yake kwa sasa, siyo Katiba,” alisema Profesa Lipumba huku akishangiliwa na wananchi.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: