BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS DKT JAKAYA KIKWETE AWATOLEA UVIVU UMOJA WA VIJANA WA CCM KWA KUWAITA MAKUWADI KISA....!.

http://i.telegraph.co.uk/multimedia/archive/01755/tan_1755068c.jpg
 

Rais Jakaya Kikwete amesema umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umegeuka jukwaa la watu wanaotaka kugombea urais kwa kuwa makuwadi na mawakala wa kuhonga fedha vijana wenzao badala ya kufanya mijadala ya kukijenga chama.


Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa shirikisho la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, mjini hapa.

Alisema vijana wa chama hicho wanatakiwa kuwa wapiganaji, wapambanaji na wanaharakati katika katika kukiimarisha chama kutokana na hatma ya CCM ipo mikononi mwa vijana wake.

“Kupata wanachama vijana kitupa fursa ya mtazamo mpya wa kimaendeleo kwa chama chetu na ninaamini kupitia shirikisho hili tutakijenga na kukiimarisha chama…Maana kule umoja wa vijana bwana umegeuka jukwaa la watu wanaotaka kugombea urais,” alisema Rais Kikwete.

Alisema badala ya umoja huo kukaa na kuzungumza mambo ya mstakabali wa chama na Taifa, lakini viongozi wa vijana ndio wanachukua fedha kwa wazee na kuwagawia vijana.

“Vijana hamuwezi kugeuka makuwadi na mawakala wa kuhonga wenzenu, ikiwa kwa namna hii watakuwa wametoka kabisa kwenye mstari maana katika kikao cha NEC nilimuita Sixtus (Katibu wa UVCCM) na wenzake nikamwambia huko mnakoenda siko, rudini huku…sisi tunategemea miaka 30 ijayo Rais atoke miongoni mwenu ni lazima tufanye kazi ya kuwaandaa vijana ili wawe viongozi wazuri,” alisema na kuongeza:

“Unaposema umoja wa vijana, utakuta viongozi wale wanasafirishwa kwasindikiza wazee wanaotaka urais, haiwezekani nyie vijana mkahusishwa na ugawaji rushwa, zamani enzi zetu hoja za vijana zilikuwa zina nguvu, lakini sasa hivi hoja za vijana sio tishio tena kwa mtu yoyote.”

Alisema kwa sasa hawatoi hoja za kukijenga chama na kuwataka kurudi nyuma na kurudisha misingi ya uanzishwaji wa umoja huo.

Rais Kikwete alisema anaamini shirikisho hilo litakipa uhai chama kwa kutoa mawazo ya kujenga matumaini mbele ya safari kwa kutambua mahitaji ya wananchi katika jamii na kuyasemea.

“Haiwezekani ukawa na viongozi wa vijana ambao wanafanyakazi ya kugawa hela ya wazee kwa vijana wenzao, jambo ambalo halifai kwani umoja huu hauwezi ukawa jukwaa la kampeni kwa wanaotafuta urais,” alisema Rais Kikwete.

Akizungumzia kuhusiana na shirikisho hilo, Rais Kikwete alisema jukumu lao kuu ni kutafutia chama wanachama, marafiki,na kuungwa mkono na wanafunzi wa elimu ya juu na wanafunzi wengine na pia kuwa kiungo muhimu kati ya CCM na wanafunzi hao.

Aidha, alisema shirikisho hilo linawajibu wa kuwa chombo cha uwakilishi wa maslahi ya wanafunzi na kuwa wepesi kuyatambua mambo yenye maslahi kwa wanafunzi na kuyasemea.

“Muwe tumaini na kimbilio la wanafunzi kwa kutatua changamoto na kuzisemea kwa chama na serikali badala ya kuacha mambo yakaharibika na kuamsha migogoro, shirikisho hili ni tanuru la kupiga viongozi wa baadaye ni lazima muwe na mipango mathubuti,” alisema.

Aliwataka kuchagua viongozi wazuri, waaminifu, waadilifu, wabunifu na wachapa kazi katika shirikisho lao ambao watakuwa na uwezo wa kujenga hoja.

Hata hivyo, alisema wawe wepesi kukubaliana na matokeo ya uchaguzi ambao wanaufanya katika shirikisho hilo kwani hata yeye mwaka 1995 kura za urais hazikutosha, lakini hakukata tamaa.

“Chama kinasema jitokezeni kugombea, nasubiri hiyo Juni 3 watajitokeza wangapi, maana ninavyosikia ni wengi wapo zaidi ya 20 wanaotaka urais, lazima tushirikiane kujenga chama chetu na shirikisho, mimi nilijaribu mwaka 1995 kugombea urais, lakini kura hazikutosha na sikumnunia Mzee Mkapa,” alisema Rais Kikwete.

Akimkaribisha mgeni rasmi mlezi wa shirikisho hilo, January Makamba, alisema shirikisho hilo lina matawi 137 katika mikoa mbalimbali nchini na kuzitaja changamoto zinazowakabili vijana hao ni mikopo ya wanafunzi, ushirikishwaji katika kampeni na suala la ajira na kumuomba Rais Kikwete kuyatafutia ufumbuzi.

Shirikisho hilo pia litafanya uchaguzi wa ngazi mbalimbali za uongozi ikiwamo nafasi ya uenyekiti, makamu mwenyekiti, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), katibu wa uchumi na fedha, katibu wa siasa na uenezi na Katibu wa uhamasishaji. CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: