Serikali imelaumiwa kuwa imeshindwa kuweka mkazo katika kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kama inavyofanya kwa wanyama kama tembo hali inayosababisha mauaji ya watu hao kuendelea nchini.
Aidha, Serikali imelalamikiwa kwa kuzitengea fedha kidogo Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Wizara ya Kazi na Ajira ambazo
haziwezi kusaidia kutekeleza miradi ya maendeleo katika wizara hizo.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Riziki Omari Juma, alisema mauaji ya
albino yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara hali inayozua maswali kwa
wananchi kuhusu mahali Taifa linapopelekwa.
Juma aliitaka serikali iweke utaratibu wa kuwalinda watu wenye
ulemavu wa ngozi badala ya kuendelea kufanya uchunguzi kusaka wahalifu
kila unapotokea uhalifu.
“Kila siku matukio ya albino kukatwa viungo na wengine kuuawa
yanatokea, lakini hatuoni serikali ikichukua hatua kuwalinda, tembo
wanalindwa sana na ikitokea ameuawa mmoja tu wahalifu wanasakwa, lakini
albino akiuawa hakuna hatua zinazochukuliwa,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Maulidah Komu.
Juma aliitaka serikali kufuatia wafanyakazi wa ndani ambao wamekuwa
wakinyanyaswa na mama na baba mwenye nyumba kwa kulipwa ujira kidogo.
Naye Mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa, alisema serikali
ianzishe utaratibu wa kuanza kutoa mikopo kwa vijana wanaomaliza darasa
la saba ili wapate fursa ya kujiunga na vyuo vya Mamlaka ya Ufundi Stadi
(VETA).
“Vijana wanaomaliza darasa la saba wengi wanashindwa kupata nafasi
ya kupata nafasi ya kujiunga na masomo VETA kwa kukosa pesa, hivyo ni
wakati sasa kwa serikali ianze kuwakopesha mikopo kama inavyofanya kwa
wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu,” alisema.
Mbunge wa Mafinga (CCM), Mendrad Kigola, alisema tatizo la ajira
kwa vijana limeendelea kuwa kubwa na sasa waliomaliza vyuo vikuu
wanaamua kujiajiri katika kazi ya kuendesha pikipiki (bodaboda), hivyo
serikali ianze kuwakopesha bodaboda.
Kigola alisema mashirika mengi ya umma yanalipa viwango vidogo vya
mishahara na kutaka serikali ifuatilie hali hiyo kwani haiwezekani
mashirika madogo ndiyo yalipe mishahara mikubwa na mashirika makubwa
yanalipa kidogo.
Alisema Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto haijamsaidia
mwanamke wa kijiji katika kupata haki zake za msingi na kusababisha
aendelee kukabiliwa na umaskini wa kiwango kikubwa.
Kigola alisema Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kazi
Duniani (ILO) yasaidie katika kuwaletea maendeleo wanawake wa vijijini
ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Maulidah Komu, alisema watoto
yatima na watoto wa mitaani serikali haijawasaidia, badala yake imekuwa
na mikakati ya muda mrefu ambayo haiwasaidii walengwa.
“Watoto yatima na wa mitaani wanapata tabu sana mfano, kuna nyumba
moja ya kuwalea ilikuwa Morogoro, walikuwa wanafanyiwa kitu kibaya
serikali haichukui hatua,” alisema.
Komu alisema inashangaza baadhi ya wabunge licha ya kutambua kero
zinazowakabili wananchi, lakini wanaunga mkono kwa asilimia 100 bajeti
za wizara, lakini wanapochangia wanaanza kuorodhesha kero lukuki
zilizopo katika majimbo yao.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment