BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UTORO WA KUTISHA BUNGENI: WABUNGE 33 TU NDIYO WALIOPITISHA MUSWADA WA BENKI YA POSTA TANZANIA DODOMA.

 

Wabunge wakiwa  ndani ya ukumbi wa  bunge  wakati wa kupitisha muswada wa Posta, Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma.
Wabunge 33 jana walipitisha Muswada wa Benki ya Posta Tanzania (kufuta sheria iliyoanzisha Sheria ya Benki ya Posta na kuweka masharti ya mpito).


Idadi ya wabunge wote ni 356 na nusu yake ni 178 wanaotakiwa kupitisha jambo lolote lenye uamuzi ikiwamo miswada.


Tangu asubuhi jana, kulionekana kuwa na idadi ndogo ya wabunge huku baadhi yao wakiingia na kutoka kila walipomaliza kusaini mahudhurio.


Mara baada ya kupitishwa kwa muswada huo ambao uliwasilishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, idadi ya wabunge ilipungua zaidi na kubaki wabunge 29 huku Muswada mwingine wa Sheria ya Masoko ya Bidhaa wa 2015 ulipokuwa ukiwasilishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima.


Wakati hali ikiwa hivyo ndani ya Ukumbi wa Bunge, kulikuwa na idadi ndogo ya wabunge walioonekana nje ya ukumbi wakizungumza kwa vikundi na wengine wakiwa ‘bize’ na simu zao za mikononi.


Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa alilalamikia kitendo hicho akisema ni uvunjaji wa kanuni na Katiba ya nchi.


Mnyaa alisema kuwa wabunge wa Tanzania wengi ni wapole na wasiopenda makuu kwani kama ingetokea mtu yeyote akasimama na kuamua kushtaki, lazima angeshinda na kupata umaarufu mkubwa.


“Hapa tunachokifanya siyo jambo jema hata kidogo, unajua mambo mengi tunayopitisha hapa yanakuwa sheria. Si sahihi na tunaanza kuvunja sheria sisi wenyewe humu ndani,” alisema Mnyaa.


Alisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 94 (1) ambayo inaeleza kuwa upitishwaji wa jambo lolote linalohusu uamuzi wa wabunge ni lazima akidi iwe ni nusu ya wabunge wote kama ilivyo Kanuni ya 77 ya Bunge.


“Kila tukisema sisi tunapingwa na kuambiwa kaa chini, tena sisi wapinzani ndiyo shida kweli na hasa hawa wanaokalia viti (anawataja) wanatubana sana ni afadhali na Ndugai (Job, Naibu Spika),” alisema.


Mbunge huyo alibainisha kuwa wakati wowote kama ataibuka mtu wa kutaka kuliburuza Bunge mahakamani, atashinda kesi hiyo mchana kweupe na sheria nyingi zitapaswa kufutwa.


Ndugai ajibu
Akizungumzia hali hiyo Ndugai alisema licha ya umuhimu wa akidi lakini jambo hilo limekuwa shida duniani kote.


Ndugai alisema katika uzoefu wake na mabunge mengi duniani ambayo ameshayaona, suala la akidi huwa ni tatizo ambalo limeshindikana kwa kuwa hakuna sheria ya kuwakamata kwa nguvu wabunge ili waweze kuhudhuria vikao.


“Kwanza kinachoangaliwa siyo kingine, bali ni jicho la Spika, mimi nimeangalia pale nikaona kwa macho yangu kuwa’ quorum’ (akidi) imetosha hivyo nikaendelea,” alisema Ndugai.


Alisema Bunge la Jamhuri pamoja na kuweka mkazo kuwa wasiohudhuria vikao hawatalipwa posho, lakini bado kumekuwa na wabunge watoro ambao kufika kwako katika Bunge ni shida.


Hata hivyo, alitetea suala la posho kwamba wakati mwingine ni kikwazo kwani licha ya Watanzania kupigia kelele posho za wabunge kuwa ni kubwa, lakini haziendani na majukumu waliyonayo ndiyo maana wanakimbilia huko nje kufanya shughuli za ujasiriamali.


Naibu Spika alisema wengi wa wabunge hufika bungeni hapo kwa kuangalia kama kuna miswada ambayo inaweza kuwa na manufaa kwao.


Siku zilizosalia
Bunge limetoa ratiba kwa siku zilizosalia katika uhai wa Bunge la 10 ambayo inaonyesha kuwa leo kutakuwa na shughuli ya kupitisha Muswada Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi wa mwaka 2015.


Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Alhamisi hadi Jumatatu kutakuwa na vipindi vya maswali na kupitishwa kwa Muswada wa Sheria ya Petroli na Muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesi wa mwaka 2015 kabla ya kuhitimisha kwa Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania.


Bunge litahitimisha kazi zake kwa kupitisha Miswada ya Sheria ya Tume ya Walimu Jumatano ijayo na Alhamisi itakuwa ndiyo siku ambayo Rais Jakaya Kikwete atalihutubia kabla ya kulivunja.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: