BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015, WIZI WA SHAHADA ZA KUPIGIA KURA WAIBUKA, MGOMBEA URAIS WA CCM ANG'AKA VIBAYA.

Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli , amewastukia watu aliowaita mafisadi wanaozunguka mitaani na kuwalaghai wananchi ili wawauzie shahada zao za kupigia kura.

Akiwahutubia wananchi hao katika mkutano wake wa kampeni kwenye mji wa Kiomboi Jimbo la Iramba Magharibi, mkoani Singida akiwa katika siku yake ya mwisho mkoani hapa, alisema mafisadi hao wakifanikiwa kununua kadi hizo hawatashindwa kuwauza wenyewe iwapo watachaguliwa kuingia Ikulu.

Aliwatahadharisha wananchi wasikubali ulaghai kwa kuwa kufanya hivyo ni kuuza haki yao ya msingi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.

“Tuna taarifa kwamba wameanza kuweka mipango ya kununua kadi za kupigia kura, msikubali ulaghai huo maana watu hao wakichaguliwa ni hatari kwa nchi, kama watanunua kadi zenu watashindwaje kuwauza nyinyi wakiingia Ikulu?” Alihoji.

Akiwa katika jimbo la Iramba Mashariki, Dk. Magufuli alimrushia kijembe aliyekuwa Mbunge wa Iramba Mashariki kwa tiketi ya chama hicho, kuwa alichelewesha maendeleo ya jimbo hilo.

Huku akimnadi mgombea wa jimbo hilo ambalo kwa sasa linaitwa Mkalama, Allan Kiula, alisema mbunge huyo aliliongoza jimbo hilo kuanzia mwaka 1995 hadi 2010 alipoangushwa kwenye kura za maoni na sasa anagombea Jimbo la Singida Mjini kwa tiketi ya Chadema.

Akizungumza bila kumtaja jina, Dk. Magufuli alisema mbunge huyo amekaa muda mrefu lakini hakuna lolote alilowachia wananchi kwani alikuwa mpiga porojo.

“Mlikosea kuchagua mbunge hapa Iramba, mbunge wen
u alikaaa muda mrefu lakini amewachelewesha, yeye alikuwa mtu wa porojo tu na ndiyo maana hivi sasa ameamua kuwakimbia na kwenda kugombea jimbo lingine kwasababu anajua angeanguka huku,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza.

“Hivi niwaulize ukiwa na paka nyumbani kwako akakimbilia porini si anabaki kuwa paka tu, sasa msifanye makosa nichagulieni Allan maana namjua kwa uchapakazi wake,” alisema.

Dk. Magufuli aliahidi kujenga nyumba za watumishi kwa ajili ya wilaya mpya ya Mkalama ili wafanyakazi wote wanaoajiriwa waishi karibu na makazi ya wananchi.

Alisema akiwa rais ataagiza kujengwa kwa nyumba za walimu ili iwe motisha kwa walimu wanaoajiriwa kufanyakazi katika Wilaya hiyo ya Mkalama.

Mgombea huyo aliwaomba wananchi wa vyama vyote vya siasa kumpa kura akiahidi kuwa atakapochaguliwa atakuwa rais wa Watanzania wote bila kubagua vyama vyao.

“Chadema mnasema people’s power, sasa hiyo power msikae nayo bure nipeni mimi Magufuli hiyo power niingie Ikulu nikawafunge mafisadi kwa makufuli yangu,” alisema Dk. Magufuli na kuamsha shangwe kwa wananchi waliokuwa wakimsikiliza.

Akizungumza na wananchi wa Singida Mjini,
Dk. alisema atakuwa akitoa vibali kwa wawezaji wanaotaka kujenga viwanda nchini ndani ya siku moja na kuwataka wale wanaovihitaji kuanza kumwona.

Alitoa ahadi hiyo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni wakati alipokuwa akimtambulisha Mbunge mstaafu wa Singida Mjini, Mohamed Dewji.

Alimsifu Dewji kuwa ni mwekezaji mzalendo ambaye amesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira nchini na kumwahidi hata akitaka kibali cha aina gani yeye yuko tayari kumpa ili ajenge viwanda vingi zaidi.

“Wewe ni mzalendo wa kweli umetusaidia sana na mimi niko tayari kukupa kibali unachotaka hata leo leo maana nina uhakika wa kupata urais, niambie unataka kujenga kiwanda gani ili nikupe kibali ukajenge,” alisema Dk. Magufuli na kufanya umati wa watu waliohudhuria mkutano huo kuangua kicheko.

Aliahidi kutengeneza soko kubwa la kimataifa la vitunguu mkoani hapa ili kuwainua wakulima wa zao hilo nchini.

Alisema ana uhakika nchi nyingi za Afrika na Ulaya zitachangamkia zao hilo.

Alisema vitunguu vinavyozalishwa mkoani Singida vina ubora wa hali ya juu hivyo atafanya awezalo kuhakikisha anawajengea soko la kimataifa wakulima kama njia ya kuwaondoa kwenye umaskini.

Alisema mbali na soko hilo, anakusudia kujenga kiwanda kikubwa cha ngozi, nyama na maziwa kitakachoongezea thamani mifugo na kuwa na fedha zitakazowasaidia kuondoa umaskini.

Dk. Magufuli alisema kukiwa na kiwanda cha ngozi hakutakuwa na haja ya kuagiza viatu wala mikanda kutoka nje ya nchi kama ilivyo hivi sasa na Tanzania itauza nje ya nchi bidhaa zitokanazo na ngozi ili kupataa fedha za kigeni.

Alisema Tanzania ndiyo inashika nafasi ya pili Afrika kwa kuwa na ng’ombe wengi wanaofikia milioni 2.4 ambao wanaweza kuipaisha nchi kiuchumi kwa kusindika nyama na kuuza nje ya nchi.

Mgombea huyo alisema vikiwepo viwanda vingi hapa nchini tatizo laa ajira litaakuwa historia kwani vijana wengi wanaomaliza vyuo vya ufundi na vyuo vingine nchini watakuwa wanaajiriwa moja kwa moja.

MWIGULU
Mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya mgombea huyo, Mwigulu Nchemba, alisema mabadiliko yanayotakiwa ni ya kiutendaji na wala si ya kubadili vyama vya siasa madarakani.

“Huyu ni mgombea pekee wa urais ambaye akisimama na kusema anachukIa rushwa kweli ukimwangalia usoni unaona andhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi, wengine kazi yao ni kupanga madili ya namna ya kuiba gesi na mafuta,” alisema Mwigulu.

MAKAMBA
Mjumbe mwingine wa timu hiyo, January Makamba, aliwaambia wananchi hao kuwa Dk. Magufuli ndiye mgombea anayeweza kuibadili Tanzania na kuwa nchi yenye uchumi mkubwa kwa kuanzisha viwanda. CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: