BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KASI YA UTENDAJI WA KAZI KWA RAIS DK MAGUFULI UNATISHA, WAMSOMBA KAMISHNA MKUU WA TRA.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa (kushoto) akikabidhi orodha ya makontena kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rished Bade (wa pili kushoto). Makontena hayo yanadaiwa kupotea bandarini bila ya viongozi wa TRA kujua. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Dar es Salaam.
Rais John Magufuli amemsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade baada ya kubaini ‘madudu’ katika ofisi za mamlaka hiyo.

Badala yake amemteua Phillip Mpango kukaimu nafasi hiyo hadi pale uteuzi mwingine utakapofanyika.

Katika hatua hiyo iliyotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Ikulu jana, Rais pia amezuia safari kwa watumishi wote wa TRA ili watoe ushirikiano katika uchunguzi wa sakata hilo.

“Mnakumbuka kuwa Rais alisema atatumbua majipu, hilo ni jipu la kwanza lakini bado uchunguzi unaendelea. Watasimamishwa zaidi kadri uchunguzi, unavyoendelea,” alisema.

Kabla ya Rais kumsimamisha Bade, Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa aliwasimamisha kazi maofisa watano wa TRA na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kuwahamisha vituo vya kazi wengine watatu, kutokana na tuhuma za ufisadi, uzembe na rushwa alizobaini.

Majaliwa jana alifanya ziara ya ghafla katika ofisi za Bandari na kuwasimamisha watumishi hao akiwamo Kamishna wa Kodi na Forodha wa TRA, Tiagi Masamaki na Habibu Mponezya wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja ambao wanatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha uliotokana na upotevu wa makontena zaidi ya 349.

Hatua hii imekuja baada ya kugundulika kuwa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya Sh80 milioni yamepotea huku TPA ikiwa na taarifa lakini hayaonekani katika mtandao wa TRA.

Wengine waliosimamishwa kazi ni Haruni Mpande na Hamis Ali Omari wote wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Eliachi Mrema wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD).

Watumishi wa TRA waliohamishwa vituo na kupelekwa mikoani ni Nsajigwa Mwandegele, Robert Nyoni na Anangisye Mtafya.

Majaliwa
Akizungumza na viongozi wa TPA na TRA katika ziara hiyo, Waziri Majaliwa alimtaka Bade na Naibu Kamishna Mkuu, Lusekelo Mwaseba kushirikiana na polisi kufuatilia upotevu wa fedha hizo na kuhakikisha kwamba zinapatikana na kurudishwa serikalini.

Kikao hicho cha dharura, kilihudhuriwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens Turuka, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Shabaan Mwinjaka, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na Mkurugenzi Mtendaji wa TPA, Awadh Massawe.

Katika kikao hicho, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Hazina, Dk Servacius Likwelile kuhakikisha anapeleka wataalamu kutoka Wakala wa Serikali Mtandao(e-govt) kukagua mifumo ya taarifa na kubaini jinsi wizi unavyofanyika kwa njia ya mtandao.

Alipohojiwa katika kikao hicho, Bade alikiri kuwa kuna upotevu wa makontena ambao kwa kawaida unafanyika kati ya bandari kuu na bandari kavu (ICD) hasa bandari kavu ya Ubungo.

“Tulifanya ukaguzi na kugundua makontena 54 yamepotea kwa njia ya wizi, tulipoendelea na ukaguzi tukagundua kuwa mengine 327 hayapo.”

Bade alisema suala hilo linafuatiliwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Alisema mmiliki wa ICD, ametakiwa kulipa faini ya Sh12.6 bilioni na mpaka sasa ameshalipa Sh2.4 bilioni.

Awali, Waziri Majaliwa alifika bandarini saa sita mchana na kuitisha kikao cha dharura kilichohusisha TPA na TRA na makatibu wa wizara ili kujadili changamoto kuhusu ufanisi na upatikanaji wa mapato.

Duka la Sapna lafungwa
Licha ya kukabiliwa na hekaheka hiyo, TRA imefanya operesheni maalumu ya kukagua wafanyabiashara ambao ni wadaiwa sugu wa kodi na kufungia maduka kadhaa makubwa, likiwamo la simu la Sapna lililopo Posta Mpya jijini hapa.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo alisema tangu tarehe Mosi, mwezi huu hadi jana, TRA imeshaokoa Sh1.9 bilioni kupitia ukaguzi huo huku wafanyabiashara 10 wakinaswa kwa kukwepa kodi ya Sh6.7 bilioni katika operesheni iliyofanyika jana pekee.

Kayombo alisema endapo wamiliki wa duka hilo la Sapna hawatalipa deni la kodi wanayodaiwa, mali za duka hilo zitapigwa mnada na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

“Kuna utaratibu wa muda wa kulipia deni la kodi ambalo hatuwezi kuliweka wazi, watakuwa salama kama wakieleza jinsi gani watakuwa wanapunguza deni hilo lakini vinginevyo tutataifisha mali zote, halafu siyo Sapna pekee wako wafanyabiashara wengi,” alisema.

Kayombo alisema operesheni hiyo itakuwa endelevu kwa nchi nzima. Alisema kodi nyingi zinapotea kutokana na udanganyifu wa wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kulipia makadirio sahihi ya kodi wanazotakiwa kujikadiria kwa mamlaka hiyo.

Kabla ya Kayombo kutoa kauli hiyo, maofisa wa mamlaka hiyo walifanya operesheni katika Mkoa wa kodi wa Ilala na kupita katika duka hadi jingine na kufunga ofisi za wafanyabiashara husika wa maeneo hayo.

Duka la Sapna lilifungwa saa tisa alasiri na maofisa hao, huku taarifa za ndani zikieleza kudaiwa mamilioni ya shilingi.

Mabasi ya UDA yakamatwa
Mbali ya kufunga duka hilo, pia maofisa wa TRA walikwenda kwenye ofisi za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), ambako walikamata baadhi ya mabasi kutokana na kudaiwa kodi.

Operesheni hiyo pia imefanyika katika eneo la Victoria ambako kuna kampuni inayohusika na uuzaji wa redio upepo na rimoti za magari. Akizungumzia kasi ya Rais Magufuli Ikulu jana, Balozi Sefue aliwataka wafanyabiashara ambao wanajijua kuwa walipitisha bidhaa zao bila kulipa ushuru wajitokeze wenyewe badala ya kusubiri Serikali iwafuate.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: