BannerFans.com BannerFans.com


Kwa masikitiko makubwa napenda kuutahadharisha umma wa watanzania juu ya kuibuka kwa mtu tapeli anayejitambulisha kuwa ni DANIEL MJEMA, Mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi.

Novemba mwaka 2013, alijitambulisha hivyo kwa Mwenyekiti wa taifa wa Chadema mhe. Freeman Mbowe na kudai eti mimi nimefiwa na mama yangu.
Kwa mila na desturi zetu, Mheshimiwa Freeman Mbowe pamoja na wabunge kama Esther Bulaya, Grace Kiwelu na wengine walihamasishana na kuchanga rambirambi inayofikia sh900,000.

Mheshimiwa Mbowe na wengine walimpigia simu mtu huyo wakimweleza walitaka kuungana nami (wakiamini ni mimi) kuaga mwili hapo Muhimbili lakini akadai walikuwa wameshaondoka na walikuwa wakielekea Moshi hivyo atumiwe rambirambi hiyo kwa M-Pesa. Alitumiwa fedha hizo.

Lakini Mhe. Grace Kiwelu alitilia mashaka namba hiyo kwa vile namba iliandika jina tofauti na langu lakini kwa bahati mbaya nilikuwa nimepumzika mchana huo.

Nilipokuta missed call yake, nilimpigia kwenye saa 12:00 jioni akaniuliza kama tulikuwa tumefika Moshi. Nilishangaa kwa vile sikuwa nimesafiri kwenda Dar karibu miezi miwili.

Ndipo akashtuka akaniambia "TUMETAPELIWA" na akanieleza hadithi niliyotangulia kuieleza.

Niliwasiliana na Mhe Mbowe akanihakikishia kuwa mtu huyo alijitambulisha kuwa ni Daniel Mjema na alitilia shaka sauti na kumuuliza mbona sauti sio yangu akajitetea ni kwa sababu ya msiba.

Haikuishia hapo, mwaka jana mtu huyo huyo akamtumia sms Dk. Emanuel Nchimbi na kujitambulisha kuwa ni Daniel Mjema wa gazeti la Mwananchi na kwamba nimefiwa na mke wangu.

Dk. Nchimbi alitilia shaka na kumpigia simu managing Editor wangu Denis Msack akiuliza kama nimefiwa na mke wangu naye akamwambia hakuna jambo kama hilo. Dk. Nchimbi akaeleza kuwa Novemba 2013 alimtumia mtu huyo sh200,000 baada ya kujitambulisha kuwa ni Daniel Mjema wa Mwanchi na kwamba nimefiwa na mama yangu jambo ambalo sio kweli. Safari hii alitakiwa tena atumiwe sh200,000.

Dk. Nchimbi alitoa taarifa Polisi na mtego uliandaliwa huko Kibaha Pwani lakini huyo mtu alikuwa smart kwani hakwenda yeye bali alimtuma mwandishi wa hapo Pwani amsaidie kupokea hizo fedha then amtumie kwa M-Pesa.

Nimeeleza kwa kirefu jambo hili kwani mtu huyo ameendelea kutapeli watu katika maeneo mbalimbali hasa mikoa ya kaskazini akibuni njia mbalimbali.

Leo niliitwa kwa Katibu wa CCM mkoa Kilimanjaro na nilipofika hapo nilimkuta akiwa na mtu mwingine akamuuliza unamfahamu huyu(Yaani mimi) yule bwana akasema hanijui na kwamba sio mimi.

Ndipo katibu akaniarifu kuwa kuna mtu ameenda kujitambulisha kwa huyo bwana kuwa yeye ni Daniel Mjema wa gazeti la Mwananchi na kumtapeli sh500,000.

Nilimshauri huyo bwana afungue taarifa Polisi ili mtu huyo aweze kutafutwa.

Ninaomba msambaze taarifa hii ili kuwasaidi raia wema maeneo mbalimbali ya nchi ambao huenda wakatapeliwa leo, kesho au kesho kutwa.

Napenda kutamka kuwa mama yangu mzazi Happyness Mjema na mke wangu mpenzi Tamari Mndeme wako hai kwa mapenzi ya Mungu.

Daniel Mjema
Mwandishi wa Habari
Gazeti la Mwananchi
Kilimanjaro.

JINA LA MWANDISHI WA GAZETI LA MWANANCHI LATUMIKA KATIKA UTAPELI

admin
,

Tangazo la Wito Chuo Cha Polisi Moshi

Tangazo la Wito chuo cha polisi moshi kwa wahitimu wa kidato cha sita mwaka 2014, kidato cha nne mwaka 2014 na JKT mwaka 2015 waliochaguliwa kujiunga na jeshi la Polisi.

Bonyeza hapa kupata majina hayo.

JESHI LA POLISI LATOA TANGAZO KWA WAHITIMU KIDATO CHA SITA, NNE NA JKT 2015 LA KUJIUNGA NA UPOLISI.

admin
,

Ratiba ya Mgombea Urais Wa CHADEMA/UKAWA MH.EDWARD LOWASSA,
29/8/2015-JANGWANI DSM.
30/08/2015-IRINGA.
Mufindi 3.00-4.30 Asubuhi,Mahali Mufindi Mjini.
Kilolo 5.30-7.00 Mchana,Mahali Ilula.
Isimani/Kalenga 8.00-9.30 Alasiri Mahali,Kalenga.
Iringa Mjini 10.30-12.00 Jioni Mahali,Mwembetogwa.
31/08/2015 NJOMBE.
Makambako 3.00-4.30 Asubuhi Mahali Makambako
Ludewa 5.30-6.30 Mchana,Mahali Ludewa Mjini.
Njombe Kusini 10.00-12.00 Jioni Mahali Njombe Mjini.
1/9/2015.RUVUMA.
PERAMIHO, 3.00-4.30Asubuhi Mahali Madaba.
Nyasa 5.30-6.30 Mchana Mahali Nyasa.
Mbinga 8.00-9.00Alasiri Mahali Mbinga Mjini.
Songea 10.30-12.00 Jioni Mahali Songea Mjini.
2/9/2015
Tunduru3.00-4.30 Mahali Tunduru.
Namtumbo 5.30-7.00 Mchana Mahali Namtumbo Mjini.
RUKWA,
Sumbawanga 10.00-12.00 Jioni Mahali Sumbawanga Mjini.
3/9/2015
Nkasi 3.00-4.30 Asubuhi Mahali Namanyere
KATAVI.
Mlele 5.30-7.0
Mchana Mahali Mlele.
Mpanda 8.00-9.30Alasiri Mpanda Mjini.

BAADA YA DAR ES SALAAM, UKAWA KUMNADI LOWASSA NYANDA ZA JUU KUSINI KAMPENI YA URAIS AGOSTI 30

admin
,
http://mtanzania.co.tz/wp-content/uploads/2015/08/mtz11.jpg
SIKU moja baada ya mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kuzuiwa na polisi kutembelea wananchi mitaani, Manispaa ya Ilala imeuzuia umoja huo kutumia viwanja vya Jangwani kufungua kampeni zao keshokutwa kwa maelezo kuwa vimewahiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD iliomba kufanya mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu katika viwanja hivyo Agosti 29.

Awali Ukawa waliomba Uwanja wa Taifa, lakini walikataliwa kwa maelezo kuwa uwanja huo ni wa Serikali na hauruhusiwi kutumika kwa shughuli za kisiasa.


KAULI YA MANISPAA YA ILALA
Jana Manisipaa ya Ilala ililieleza MTANZANIA kwamba CCM, tayari waliomba kutumia viwanja vya Jangwani Agosti 23 kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni zao na siku tatu zaidi kuanzia Agosti 28 hadi 30 kwa matumizi mengine ya kisiasa.

Ofisa Utamaduni wa Manispaa ya Ilala, Claud Mpelembwa alisema kuwa Ukawa walichelewa kuomba viwanja hivyo, kwani CCM licha ya kuvitumia Agosti 23, wameviomba tena Agosti 28, 29 na 30 kwa ajili ya shughuli zao za kisiasa.

“Hatujawanyima uwanja, hata barua tuliyowaandikia wanayo inajieleza. Unajua Jangwani ni mojawapo ya maeneo ya wazi, mtu yeyote anaweza kuomba. Ukawa wao waliomba Uwanja wa Taifa na baada ya kukataliwa hawakuleta maombi kwetu.

“CCM waliomba kutumia Agosti 21, 22 na 23 na kisha wakaomba tena kutumia Agosti 28, 29 na 30. Chadema wamekuja kuomba Agosti 24. Walipokuja tukasema basi tukae tuongee, tunaweza kuwapatia Septemba 3,” alisema Mpelembwa.

Alisema kwa kuwa ndiyo kwanza kampeni zimeanza, bado wanaweza kuzungumza ili wapewe tarehe nyingine.

Hata alipoulizwa kuhusu ratiba ya kampeni inayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inayoviongoza vyama vya siasa kufanya kampeni mkoa kwa mkoa, Mpelembwa alisema ratiba hizo huwa hazipelekwi kwenye manispaa.

“Hizo ratiba huwa NEC hawatuletei, bali ni vyama ndivyo vinakuja na maombi ya viwanja… kwa kuwa huu ni mwezi Agosti, kampeni bado zinendelea hadi Septemba na Oktoba, waje tu kuomba. Siyo dhamira yetu kuwanyima uwanja,” alisema Mpelembwa.

MKURUGENZI NEC
Alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani, Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhan Kombwey, alisema bado hawajapata taarifa kutoka Chadema kuhusu kunyimwa kufanya uzinduzi wa mkutano wa kampeni kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.

“Bado sijapata taarifa yoyote kutoka Chadema kama kuna tatizo kama hilo, ngoja niwasaliane kwanza na Chadema pamoja na Manispaa ya Ilala halafu nitakupatia jibu sahihi,” alisema.


UWANJA WA TAIFA
Hivi karibuni Serikali ilikataa ombi la Chadema la kutumia Uwanja wa Taifa kuzindulia kampeni zake.

Akitoa majibu ya Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Assa Mwambene, alisema kwa mazingira ya sasa hayaruhusu kutumika kwa uwanja huo kwa ajili ya mihadhara ya vyama vya siasa.

“Kwa kipindi hiki haturuhusu Uwanja wa Taifa kutumika kwa mihadhara ya kampeni za vyama vya siasa. Uamuzi huu unalenga kuweka uwanja katika mazingira rafiki ya michezo na kuepuka athari zozote zinazoweza kujitokeza kutokana na mihemuko ya kisiasa.

“Ni kweli kwamba tulipata barua ya Chadema kuomba Uwanja wa Taifa kutumika kwa ajili ya mhadhara wa kisiasa wa Chadema, hasa kuzindua kampeni zao kwenye uwanja, tayari tumeshawaandikia kuwaarifu kuwa uwanja ule hauwezi kutumika kwa ajili ya shughuli zozote za kisiasa,” alisema Mwambene.

JAMES MBATIA
Awali kabla ya kutolewa kwa kauli ya Manispaa ya Ilala, Mwenyekiti mwenza wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema mkutano huo uko palepale hata kama wamezuiwa.

Mbatia pia alilalamikia kitendo cha vyombo vya usalama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuingilia harakati zao za siasa huku vikiipendelea CCM.

“Sasa tunasema tutazindua kampeni zetu Jangwani kama tulivyopanga. Tumefuata taratibu zote, tumeandika barua, lakini tulipotaka kulipia, tukaambiwa kuna watu wameshaomba lakini hawataki kumsema,” alisema Mbatia na kuongeza:

“Tulifuata taratibu zote baada ya kunyimwa Uwanja wa Taifa ambao uko kwa ajili ya shughuli mbalimbali, na ni kwa ajili ya Watanzania wote…Ukisema uchaguzi ulio huru na wa haki siyo siku ya kupiga kura tu bali hata mambo kama haya.”


MIZENGWE KILA KONA
Mbali na kuzuiwa kutumia viwanja vya Jangwani kuzindulia kampeni zao, Mbatia alilalamikia upendeleo unaofanywa na viongozi wa Serikali na vyombo vya dola kwa CCM huku vikikandamiza vyama vya upinzani.

“Kwa sheria ya sasa, chama tawala (CCM) kinashiriki uchaguzi kama chama dola. Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alikataza mikutano na mikusanyiko ya vyama vya siasa kwa kuwa vyama vyote vimetia saini maadili. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam naye alisema anatii agizo la mkuu wake wa kazi,” alisema Mbatia na kuongeza:

“Jumapili Mkuu wa Mkoa Sadiki alikuwa Jangwani kwenye mkutano wa CCM uliofanyika hadi saa moja kasoro wakati ulitakiwa uishe saa 12 kamili jioni. Kamanda Kova naye alikuwepo na alipigia saluti uvunjwaji wa sheria na taratibu. Nilimpigia IGP Ernest Mangu simu kumweleza.”

Alisema katika mkutano huo, Rais Jakaya Kikwete alisimamia uvunjwaji wa sheria na taratibu huku kukiwa na lugha chafu zilizotolewa na viongozi wa CCM, akiwamo Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyesema “watu wanaotaka kuleta ukombozi wa kisiasa ni wapumbavu na malofa”.

Huku akitaja matukio mbalimbali, Mbatia alisema hujuma zilianza muda mrefu ambapo Agosti 12, mgombea urais wa Ukawa, Lowassa, akiwa na msafara wake walizuiwa kwenda kumzika kada wa zamani wa CCM, Peter Kisumo wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.

“Kampeni zimeanza, mgombea wetu anakwenda kuangalia hali za wananchi na masoko mitaani. Leo alitakiwa aende hospitalini, wamemzuia. Mbona mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu jana alikwenda kutembelea hospitali? Hivi mimi nikitaka kwenda sokoni lazima niombe kibali? Mbona Mkurugenzi wa NEC hamzungumzii Samia? Mbona hazungumzii CCM kupitisha muda wa mkutano?

“Hivi karibuni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alitoa kauli za kuudhi kwa Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo, naye alimsamehe. Lakini polisi walimkamata na kumfungulia kesi. Mbona viongozi wa kitaifa wametukana matusi na hawakamatwi?” alihoji Mbatia.

MATUMIZI YA HELIKOPTA
Juzi, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeonya kuhusu matumizi ya helikopta maeneo ya hatari na mikusanyiko ya watu katika kipindi cha uchaguzi.

Chadema imekuwa ikitumia helikopta katika harakati zake za siasa tangu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kwenye chaguzi ndogo na operesheni zake mbalimbali za kisiasa.

Mwaka 2010, CCM nayo ilifuata nyayo za Chadema na kutumia helikopta kwenye uchaguzi mkuu na ikatumia tena katika mchakato wa kupata mgombea wake wa urais mwaka huu.

Hata hivyo, mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema hatatumia helikopta katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu.

Katika taarifa yake, Kaimu Mkurugenzi wa TCCA, Charles Chacha, ameonya matumizi ya helikopta katika kampeni za uchaguzi kwa maelezo kuwa kuna uwezekano wa kuleta athari za kiusalama.

“Mamlaka inatambua kwamba matumizi ya helkopta wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 yanatarajiwa kuongezeka na kuna uwezekano wa kuleta athari za kiusalama kwa maisha ya watu na mali pamoja na watumiaji wa vyombo hivi.

“Pia vitendo vya kuning’niza vitu kama mabango ya matangazo mbalimbali kwa kutumia ndege (helkopta ikiwamo) yanaweza kuleta hatari endapo sheria na taratibu zinazohusiana na matumizi hayo hazitazingatiwa,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imezungumzia mahitaji ya jumla ya kiuendeshaji, usalama wa eneo la kutua na kuruka, usimamizi wa chombo kikiwa angani na usalama kwa umma, kuchukua na kuangusha vitu ardhini na kupeperusha mabango angani na kutoa taarifa za matukio.

DONDOO MUHIMU
Agosti 23: Mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM ulipitisha muda hadi saa 12: 40 wakati muda sahihi ni saa 12:00. Katika mkutano huo, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alitoa kauli za kuudhi akisema ukombozi wa nchi umeshapatikana kupitia kwa vyama vya TANU na ASP, hivyo wanaotafuta ukombozi sasa ni wapumbavu na malofa.

Si NEC, Jeshi la Polisi wala Msajili wa Vyama vya Siasa aliyekemea au kutoa adhabu kwa vitendo hivyo vya CCM

Agosti 24: Mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa, alipanda daladala kutoka Gongo la Mboto na kwenda Mbagala jijini Dar es Salaam kujua hali za wananchi mitaani na Agosti 25 akatembelea masoko ya Tandale, Tandika na Kariakoo, na siku hiyohiyo polisi wakapiga marufuku ziara zake hizo.

Agosti 25: Lowassa alipanga kutembelea baadhi ya hospitali za umma Agosti 26, lakini siku moja kabla -Agosti 25, Wizara ya Afya ikatoa tamko la kukataza wagombea kwenda hospitali.

Wakati ikitoa tamko hilo, Agosti 25 hiyohiyo, mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu, aliwatembelea wagonjwa katika Hospitali ya Huruma, Rombo mkoani Kilimanjaro.

MGOMBEA URAIS KUPITIA UKAWA AKUMBWA NA VIZINGITI VYA KAMPENI KILA KONA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBA MWAKA HUU.

admin
,
Kocha wa timu ya Simba ,Dylan Kerr .


Dar es Salaam.
Mafanikio ambayo klabu ya Azam imeyapata kwenye mashindano ya Kombe la Kagame mwezi uliopita kwa kucheza mechi sita bila kuruhusu bao, yameishawishi Simba kuiga mfumo huo.

Timu hiyo ambayo sasa hivi inahangaika kupata kikosi bora cha kwanza kitakachoiwezesha kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu msimu huu, imeamua kujaribu mfumo wa 3-5-2, unaotumiwa na Azam inayosifika kwa kuwa na ukuta wa chuma.

Simba ambayo tangu kuwasili kwa kocha Dylan Kerr imekuwa ikitumia mfumo wa 4-4-2 na kuwachezesha, ilianza kujaribu mfumo huo wa 3-5-2 kwenye mechi dhidi ya Mwadui, Jumatatu ambayo ilimalizika kwa sare ya 0-0.

Hata hivyo, mfumo huo unaohitaji mabeki wawili wa pembeni wenye uwezo mkubwa wa kushambulia na kurudi nyuma kuzuia kwa haraka kama ilivyo kwa Shomari Kapombe, Erasto Nyoni ulionekana kuipa shida timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi iliyowakosa nyota wake kadhaa waliomo Taifa Stars.

Kocha anapotumia mfumo wa 3-4-3 hupendelea kuwatumia Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto na Ibrahim Ajibu kwa pamoja kutokana na uwezo wao wa kumiliki mpira na kupandisha mashambulizi kwa haraka.

Hata hivyo kocha anapotumia mfumo wa 4-4-2 hupendelea kuwachezesha Majabvi, Awadhi Juma na Kazimoto katikati huku akimtumia Peter Mwalyanzi kama kiungo wa pembeni lakini anayekuja katikati pia ili kuwapa uhuru mabeki wake wa pembeni, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Hassan Kessy kusaidia mashambulizi kupitia pembeni.

Wakati mwingine kocha anapotumia kikosi cha pili huwatumia Awadhi Juma, Abdi Banda pekee katikati huku katika winga akiwachezesha Issa Ngoah na Simon Sserunkuma ambao pia huingia katikati. Hii ni katika mfumo wa 4-4-2.

Beki mpya wa Simba, Emery Nibomana aliliambia gazeti hili kuwa mfumo 3-5-2 ni miongoni mwa ile ambayo klabu yao itaitumia kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

“ Huu ni mfumo mpya ambao kocha wetu atautumia pia kwenye ligi. Unapoingia kwenye ligi huwezi kutegemea mfumo mmoja na ndiyo maana kama unavyoona leo tumecheza huu wa mabeki watatu ambao naamini tutauzoea haraka,” alisema Nibomana, raia wa Burundi.

Naye kiungo mzoefu, Mwinyi Kazimoto alisema kuwa japo timu hiyo haikuumudu vyema mfumo huo wa 3-5-2, anaamini kuwa ni mzuri na utaweza kuisaidia timu hiyo kwa kiasi kikubwa siku za usoni.

“Mnapocheza viungo watano katikati mnakuwa na nafasi kubwa ya kutawala mpira na kuwanyima wapinzani nafasi ya kucheza . Ni kweli siku ya kwanza umeonekana kutupa shida, lakini ndiyo maana ya kucheza mechi za kirafiki,” alisema Kazimoto.

Iwapo Kerr ataamua kuendelea na mfumo huo, atakuwa amefuata nyayo za Mwingereza mwenzake wa Azam, Stewart Hall ambaye tangu aliporudi kuinoa klabu hiyo amekuwa akiutumia mfumo huo ambao umeifanya timu hiyo kuwa ngumu kufungika.MWANANCHI

KOCHA MKUU WA KLABU YA SIMBA SC AIGA MFUMO WA UFUNDISHAJI WA KLABU YA AZAM FC.

admin
,


SIASA: UJUMBE KUTOKA KWENYE KATUNI ALHAMISI AGOSTI 27/ 2015

admin
,
Wegesa na Nyanswi. Ni wanawake wawili kutoka kwa jamii ya Wakuria.

Wameoana kwa miaka 15 ambapo wajane wasio na mrithi wa kiume hawawezi kurithi mali huku Wagesa akimuoa Nyanswi kama mkewe ili kutatua tatizo hilo.

Nyanswi ana wavulana kwa hivyo anaweza kurithi kutoka kwa Wagesa.

Wanandoa hao wana wavulana sita,waliozaliwa na ndugu za marehemu mumewe Wagesa.

Utamaduni huu pia ni njia ya kuepuka ghasia za nyumbani ambapo asilimia 60 ya wanawake katika eneo hilo wameshuhudia ghasia za vita ama zile za kihisia.BBC

WAKURIA WAPITISHA NDOA YA JINSIA MOJA TANZANIA: WANAWAKE WAOWANA WENYEWE KWA WENYEWE

admin
,
Mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli akiwahutubia wakazi wa Tunduma kwenye mkutano wake kampeni jana. Picha na Adam Mzee

Mbeya/Hai. Mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli ameanza kuonja shubiri ya kuwanadi baadhi ya wabunge wa chama hicho baada juzi, akiwa Kalambo mkoani Katavi, baadhi ya wananchi kuguna pale alipompandisha jukwaani mgombea ubunge wa jimbo hilo, Josephat akimnadi mgombea huyo.

Kwa nyakati tofauti tangu aanze kampeni mikoani, mgombea huyo amekuwa akiwaambia wananchi kuwa baada ya kumchagua yeye, wawachague wabunge hao na kuwasamehe makosa yao ili apate urahisi wa kuunda Serikali na kuleta maendeleo.

Alisema anatambua wakati wa mchakato wa kura za maoni, kulikuwa na wagombea wengi wa ubunge lakini wananchi wasife moyo kwa sababu kuna kazi nyingi za kufanya iwapo atachaguliwa kuwa rais.

Ili kumaliza kabisa miguno iliyokuwapo, Dk Magufuli alimwita mmoja wa waliokuwa wagombea wa ubunge ili kuwaeleza kuwa anamuunga mkono Kandege na alipopanda jukwaani na kusalimia wananchi walimshangilia kwa nguvu.

Akiwa Sumbawanga Mjini juzi, Dk Magufuli alimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Aeshi Hilaly kwa kumuita jembe huku akiwataka wananchi “wampigie tena kura hata kama amewakosea.”

“Nimesema hatuchagui malaika kila mtu ana kasoro zake. Tuache kasoro, tuangalie maendeleo. Nataka Sumbawanga muwe maalumu mkinichagulia huyu (Aeshi),” alisema Dk Magufuli wakati akihutubia katika Uwanja wa Nelson Mandela juzi.

Katika Jimbo la Kwela – Rukwa, aliwataka wananchi wamsamehe mgombea ubunge, Ignas Malocha kwa makosa aliyowatendea na kuwa atafanya kazi vizuri kwenye utawala wake. “Msianze kugombana baadaye mkakosea kwa kumchagua mtu mwingine kwa sababu nahitaji mtu atakayeniambia shida katika wilaya yake.


 Hatuchagui malaika ndugu zangu, hatuchagui sura, hata mimi sura yangu ni mbaya sana na nywele zinatoka lakini Watanzania wamenichagua,” alisema Dk Magufuli akiwa katika Kijiji cha Laela. “Tumsamehe, tumjaribu afanye kazi mimi nikiwa rais tuone kama hatafanya kazi vizuri.”

Kauli hiyo ya kumnadi Malocha ilijitokeza tena alipokuwa Kata ya Lusaka aliposema wampigie kura hata kama amewakosea, wamsamehe ili apate kiunganishi kwani asipopita atashindwa kufanya kazi.

“Wewe nenda tu hata kama humpendi fumba macho lakini umpigie nani?” aliuliza Dk Magufuli na kujibiwa “Malochaaa”

Baadhi ya wakazi wa Laela walimwambia mwandishi wetu kuwa wanampenda Dk Magufuli lakini Malocha hajawatekelezea ahadi nyingi alizotoa. Akiwa katika Jimbo la Momba mkoani Mbeya, Dk Magufuli alimpigia kampeni kwa muda mrefu mgombea wa CCM, Dk Lucas Siame na madiwani wa eneo hilo na kuwataka wananchi wasifanye makosa safari hii, bali wachague chama tawala.

Akihitimisha ziara yake mkoani Rukwa, Dk Magufuli aliahidi kuanzisha mamlaka maalumu ya kusimamia masilahi ya polisi.

Akizungumza na wakazi wa Mji wa Laela, Dk Magufuli alisema anataka kuboresha masilahi ya askari ili waache vitendo vya rushwa na kudhibiti wimbi la majambazi na wizi... “...unamwona huyo ofisa amekonda kama mimi ni kwa sababu anafanya kazi,” alisema Dk Magufuli huku akimwonyesha mmoja ya polisi waliokuwapo mkutanoni hapo.

Alisema atawaongezea mishahara hata wafanyakazi wengine ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuondoa vitendo vya kutamani rushwa na kuwaonea wanyonge.

Tofauti na siku tatu zilizopita, msafara wa mgombea huyo ulisimama mara nyingi kusalimia wananchi, hasa baada ya baadhi ya wanavijiji kufunga barabara ili awasalimie.

Hata hivyo, aliposimama katika Kijiji cha Ndalambo wilayani Momba jana, kilizuka kikundi cha vijana wasiozidi 40 na kuanza kunyoosha vidole kwa alama ya V inayotumiwa na Chadema na wakati Dk Magufuli akiendelea kumwaga sera kikundi hicho kiliendelea kupiga kelele na kupinga baadhi ya ahadi kuwa hataweza kuzitekeleza huku wengine wakisema “Lowassa, Lowassa.”

Hata hivyo, mgombea huyo hakuwajali na kuendelea kuwahutubia waliokuwa wakimsikiliza na kumshangilia hasa aliposema ataunda Serikali na kuleta maendeleo ambayo hayatabagua watu kwa itikadi za vyama, dini, makabila wala mahali watokako.

Katika eneo la Tunduma alipata mapokezi makubwa hadi akasema: “Mapokezi haya ni ya hatari, ni tsunami. Kama ni ya namna hii leo nitalala kwa raha.”

Samia apata wakati mgumu Hai

Mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan jana alipata mapokezi kiduchu katika wilayani ya Hai ambayo ni ngome ya Chadema. Mkutano wake ulianzia Machame Kaskazini ambako msafara wake ulisalimiana na makada wachache wa CCM.

Hai ni jimbo lililokuwa chini ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye anawania tena kiti hicho akichuana na dhidi ya Danstan Mallya wa CCM.

Baada ya kuona msafara huo umepokewa na watu wachache, baadhi ya viongozi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro waliamua kwenda katika Sekondari ya Machame na kuwataka walimu wawatoe wanafunzi madarasani ili wahudhurie mkutano huo.

Hata hivyo, dakika tano baada ya wanafunzi hao kufika mkutanoni, baadhi ya makada wa chama hicho waliokuwa kwenye msafara wa Samia, waliwakataa na kutaka warudi madarasani kuendelea na masomo.

“Huu ni wakati wa masomo wanafunzi hawatakiwi kuwepo mahala hapa sasa,” alisema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Juma Idd.

Kitendo cha kuitwa na kurudishwa darasani, kiliwakera baadhi ya wanafunzi hao ambao walisikika wakilalamika kwamba wamewapotezewa muda wao wa masomo.

“Kwa nini wametupotezea muda wetu?,” alihoji mmoja wa wanafunzi hao.

Mmoja wa wakazi waliohudhuria mkutano huo, Vivian Mwasha alimwambia mwandishi wetu kuwa hali hiyo ilitegemewa kwa kuwa Hai ni ngome ya Chadema.

Mwasha alieleza pia kuwa inawezekana mapokezi hayo yamesababishwa na wakazi wengi wa eneo hilo kuwapo kazini asubuhi. Hali hiyo ilijirudia Masama Mashariki. 


Hata hivyo Samia hakukata tamaa, badala yake aliendelea na mkutano wake, akiwaahidi wakazi kuwa kipaumbele chake ni elimu.MWANANCHI

MGOMBEA URAIS WA CCM DKT JOHN MAGUFULI AANZA KAZI KWA UGUMU NA KUONJA ADHA YA KUWAOMBEA KURA YA NDIYO WABUNGE WA CHAMA HICHO KATAVI.

admin
,
Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewapooza wagombea wa chama hicho waliodondoshwa kwenye kura za maoni kwa kuwaahidi atawapa ajira hivyo kuwataka wasikikimbie chama hicho.

Hali kadhalika, Dk. Magufuli amewataka wana-CCM hao kutoendeleza makundi kwa kuwa yatahatarisha ushindi wa chama hicho.

Aidha, amewaombea msamaha wagombea wa Majimbo ya Sumbawanga Mjini, Kwela, Kalambo mkoani Rukwa na Momba mkoani Sogwe.

"Nawaomba muwasamehe saba mara sabini kwa kuwa hawachagui malaika bali binadamu ambaye siyo mkamilifu," alisema Dk. Magufuli.

Alisema yawezekana yapo ambayo hawakuyatekeleza kama inavyotakiwa na makosa mengine ambayo yamekuwa kinyume na matarajio ya wananchi, lakini anawahitaji afanye nao kazi na ahadi zote watakazoahidi watazitekeleza kwa maendeleo endelevu ya wananchi.

ATAKA MAKUNDI YAVUNJWE
Akiwa Jimbo la Kwela ambalo mgombea wake ni Ignus Malocha, alisema kura za maoni zimeisha na kinachotakiwa ni kuvunja makundi na kufanya kazi ya kuipa ushindi CCM.

"Inawezekana mbunge wenu hakufanya hadi mlipotarajia, namuombea msamaha kweli kweli, nipeni, huyu ni binadamu hatuchagui malaika, mchagueni Malocha msihadaishwe na maneno mengi," alisisitiza.

Akiwa Jimbo Kalambo ambalo mgombea wake ni Josephat Kandege, alisema waliobwagwa kura za maoni hawapaswi kulalamika na kuacha kuunga mkono mgombea aliyepita, kwani akiwa rais nafasi za kazi zitakuwa nyingi kila mmoja atapata.

"Nakwenda kuwa rais, nafasi za kazi ni nyingi sana. Mligombea kwa kuwa mnataka kufanya kazi, nitawapa kazi, lakini hakikisheni huyu anashinda," alisema.

Katika Jimbo la Momba ambalo mgombea wake ni Dk. Lucas Siyame, alirejea ombi la msamaha kwa wananchi hao kwa kuwa mgombea huyo alihimiza ujenzi wa barabara ya Sumbawanga hadi Tunduma, lakini kwa sababu ambazo hazieleweki walimuangusha.

"Tunaambiwa tusamehe saba mara sabini, kama kuna dhambi aliifanya msameheni na ikifika Oktoba 25, mmpe kura za ndiyo," alisema.

Alisema wagombea wengine wasiwe na shaka kwani serikali ya awamu ya tano itakuwa na nafasi nyingi za wachapakazi na waadilifu na kutokana na nia yao ya kutumikia watu, hawatakosa nafasi hizo.

"Licha ya jitihada za wakati huo, lakini mkampiga chini, ila namuombea msahama, mrudisheni wakati huu nifanye naye kazi, tunahitaji maendeleo bora kwa wote na hayo yataletwa na mafiga matatu kwa maana ya diwani, mbunge na rais," alisema.

Dk. Magufuli alisema kufanya kosa siyo kosa bali kosa kurudia kosa.

Akiwa Jimbo la Sumbawanga Mjini ambalo mgombea wake ni Aeshi Hilary, pia aliwaomba wananchi wafute makosa na kuanza upya kwa kumpa kura za ushindi.

Akiwa Jimbo la Mpanda Mjini, alitoa ahadi ya kazi kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kipindi kilichopita kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Said Arfi, na kuangushwa kwenye kura za maoni za CCM, huku akisema alikokuwa alikuwa amekosea njia.

"Kazi zipo nyingi nitakuwa rais wa nchi hii, kazi zipo nyingi wala usiwe na shaka, sitakosa nafasi ya kukupa, najua uwezo wako katika kazi," alisistiza.

Akihutubia wananchi wa eneo la Nzokala, Lusaka na Laela, alisema katika mchakato wa kumsaka mgombea urais wa CCM walikiwa 38, lakini alichaguliwa kupeperusha bendera ya chama hicho lakini wamevunja makundi na kumuunga mkono.

Aliagiza wagombea hao kupeleka orodha ya wagombea wote wa kura za maoni kwenye majimbo yao kwa ajili ya kuwapatia kazi baada ya kuingia Ikulu.

Aidha, alisema ahadi zote anazotoa atatekeleza na kwamba kubwa kwake ni utekelezaji wa huduma za jamii kama ujenzi wa zahanati vijiji vyote, vituo vya afya kwenye kata, hospitali wilayani na hospitali za rufaa mikoani na kuhakikisha dawa zinakuwapo na siyo maduka binafsi kuwa na dawa na maeneo ya umma kukosa dawa.

Alisema atahakikisha huduma ya umeme, majisafi na salama vinapatikana kwas kuwa kama aliweza katika ujenzi wa barabara, hivyo mengine hatashindwa.

ASKARI KUBORESHEWA MISHAHARA
Dk. Magufuli aliahidi kuwa akishinda katika nafasi hiyo, ataboresha maslahi ya askari ili wasiendelee kuomba rushwa kwa kuwa watakuwa na maslahi mazuri.

BARAZA DOGO LA MAWAZIRI
Aidha, alisema Baraza lake la mawaziri litakuwa dogo la kuhudumia Watanzania.

Akihutubia wananchi katika uwanja wa Nelson Mandela, Jimbo la Sumbawanga Mjini, Dk. Magufuli alisema Baraza la Mawaziri atakalounda litakuwa na mawaziri wachache na wenye kuwajibika kwa wanyonge na katika kuwapata atawachambua pole pole.

Alisema katika hilo, hatafanya usanii bali kweli tupu kwa kuwa anajua kuna maisha baada ya dunia na kwamba anataka kutekeleza ahadi zake zote kwa Watanzania ili siku atakapokufa awe rais wa malaika mbinguni.

"Sijagombea urais kwa majaribio, bali kuleta maendeleo, yapo mengi yamekwama kwa sababu ya watendaji kutotekeleza wajibu wao vizuri, wapo viongozi wala rushwa na majizi wanaosababisha huduma za wananchi zinakuwa chini," alisema.

Alisema amekuwa waziri kwa miaka 20 na akiwa Waziri wa Ujenzi, amejenga kilomita 17,762 za barabara kwa kiwango cha lami, madaraja 12,000 kati yake makubwa ni 110, madaraja mapya makubwa yanayojegwa ni 16,000 na madogo 7,200.

Aidha, alisema fedha za mfuko wa barabara miaka 10 iliyopita zilikiwa bilioni Sh. 73 na kwa mwaka huu zimeongezeka hadi kufikia Sh. bilioni 866.63 lakini tatizo kubwa ni viongozi walafi kuzitafuna.

Pia aliahidi kujenga kwa kiwango cha lami kilomita 231 za barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga, kilomita 112 za barabara ya Sumbawanga hadi Kasana na nyingine ni Sumbawanga -Mpanda -Uvinza ili kurahisisha maendeleo ikiwamo kufanya biashara na nchi za Uganda, Kenya na nyinginezo. SOURCE: NIPASHE

MGOMBEA URAIS WA CCM DKT JOHN MAGUFULI KUWAPA NEEMA WALIODONDOSHWA KATIKA KURA ZA MAONI KWA KUWAPA AJIRA.

admin
,
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.

KUTOKA KWENYE MAGAZETI YA HARDNEWS ALHAMISI AGOSTI 27/ 2015 YAKIWA NA VICHWA VIKUU VYA HABARI.

admin
,
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.

KUTOKA KWENYE MAGAZETI YA MICHEZO NA BURUDANI ALHAMISI AGOSTI 27/ 2015 YAKIWA NA VICHWA VIKUU VYA HABARI.

admin
,
Previous PostOlder Posts Home