BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

JUMA AWACHARAZA VIBOKO WALIMU WA SHULE YA MSINGI TABORA, KISA MTOTO WAKE KURUDISHWA NYUMBA ILI AKASHONE KAPTURA ILIYOCHANIKA !!!.

 
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda

VITENDO vya baadhi ya wazazi, kudhalilisha walimu vinaendelea, ambapo mzazi mmoja Selemani Juma, amewashambulia walimu wawili kwa viboko.


Amefanya hivyo kupinga mwanawe kurudishwa nyumbani, akashone kaptura. Alifanya hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Taarifa zilizofikia gazeti hili zilibainisha kuwa Juma alidhalilisha walimu wawili wa Shule ya Msingi Nzogimlole iliyopo wilayani Nzega mkoani Tabora. Aliwashambulia kwa viboko, akipinga kitendo cha mwalimu mmojawapo, kumrudisha nyumbani mwanawe.

Gazeti hili lilifika katika shule hiyo, yenye walimu tisa tu na kuzungumza na Mwalimu Mkuu Msaidizi, Emmanuel Josephat, ambaye alisema mwanafunzi huyo, Shaaban Maziku anayesoma darasa la pili, alipeleka ujumbe tofauti na alioagizwa na walimu kwa baba yake, hivyo kusababisha kadhia hiyo.

Kwa mujibu wa Mwalimu Josephat, mwalimu aliyedhalilishwa (jina limehifadhiwa), alikuwa akifundisha katika darasa hilo na alipomuona mwanafunzi huyo kavaa kaptura iliyochanika vibaya, kiasi cha sehemu za siri kuonekana, alimrudisha nyumbani kwenda kurekebisha sare yake.

Mwalimu Josephat alisema mwalimu huyo wa kiume wa darasa la pili, alimwagiza mwanafunzi wake aende kwa baba yake, akamuombe amsaidie kushona kaptura hiyo.

‘’Mwalimu hana kosa, kwani mtoto kaptura yake ilikuwa imechanika vibaya kiasi cha sehemu zake za siri kuonekana… walimu hatupaswi tuwaache hivi watoto, mwalimu alichofanya ni kumwambia akamwambie baba yake aishone ile sare, lakini mambo hayakuwa hivyo,’’ alisema Mwalimu Josephat.

Akizungumza kwa majonzi, Mwalimu Josephat alisema mtoto huyo alipofika nyumbani, alimweleza baba yake kuwa mwalimu huyo, amechana kaptura hiyo na amemwagiza arudi nyumbani kwenda kumwambia baba huyo aishone.

Ujumbe huo unadaiwa kusababisha mzazi huyo, kufika shuleni na kuanza kutoa lugha chafu dhidi ya mwalimu huyo na baadaye baba huyo alianza kutoa kipigo.

Mwalimu Josephat alidai kuwa baba huyo, alianza kutumia mawe kurusha kwa walimu hao. Baadaye alitumia fimbo, kumchapa mwalimu huyo wa darasa la pili.

Hatua hiyo inadaiwa ilisababisha mwalimu huyo, kupiga mayowe kuomba msaada. Wananafunzi waliokuwa darasani, walitoka na kuanza kumsaidia kupiga kelele za kuomba msaada.

Mayowe hayo yalisaidia mwalimu mwenzake, Elias Kafiku kutoka ofisini kwa nia ya kuamua ugomvi huo ili wazungumze kiofisi na kufikia muafaka.Lakini, mwalimu huyo pia aliambulia kipigo.

Kutokana na kipigo hicho, mwalimu huyo wa darasa la pili alipata majeraha na kupelekwa zahanati ya kijiji, ambako alipatiwa huduma na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Akizungumza na gazeti hili, mwalimu huyo wa darasa la pili alisema hali yake inaendelea vizuri. Alisema sababu ya kupigwa na mzazi huyo, hazijui kwa kuwa alitekeleza majukumu yake kama kawaida.

Akitoa maoni yake kuhusu tukio hilo, Mwalimu Elizabeth Kafulila wa shule hiyo, alisema tukio hilo limewatia hofu katika utendaji kazi, kutokana na mzazi kuingilia majukumu ya walimu.

Mwalimu Elizabeth aliwataka wazazi kujirekebisha na kushirikiana na walimu katika kulea watoto wao, na wanapokuwa na malalamiko, wafuate taratibu za kiofisi.

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda alisema mzazi huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kupiga na kujeruhi vibaya na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: