BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MABOMU 7 YA KUTUPWA KWA MKONO YAKAMATWA KATIKA JIJI LA ARUSHA HUKU WATU 25 WAKISWEKWA LUPANGO.


Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu (kushoto)akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana watu waliokamatwa na mabomu saba mjini Arusha. Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas.Picha na Filbert Rweyemamu.

Arusha.
 

Jeshi la Polisi limekamata mabomu saba ya kutupa kwa mkono, risasi sita za bunduki aina ya Shortgun, mapanga mawili na bisibisi moja, katika operesheni dhidi ya matukio ya mabomu mjini hapa.


Jeshi hilo pia linawashikilia watu 25 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya milipuko ya mabomu katika nyumba za ibada, mkutano wa hadhara wa Chadema, mgahawa na nyumba za viongozi wa dini. Mabomu hayo yamekamatwa eneo la Sombetini nyumbani kwa Yusufu Ali (30) ambaye pamoja na mkewe Sumaiya Juma (19) wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.


Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu alisema jana kuwa mabomu sita yaliyokamatwa yametengenezwa Urusi wakati moja limetengenezwa Ujerumani.


“Tunaowashikilia wanatuhumiwa kuhusika na matukio ya milipuko ya mabomu kuanzia ile ya Kanisa la Olasiti na mengine yaliyofuata,” alisema Mngulu.


Alisema hadi sasa polisi imefanikiwa kubaini mtandao wa wahusika wa matukio ya mabomu nchini na inawasaka watu wengine 25 kwa tuhuma za kuhusika na mtandao huo.


Licha ya kudai polisi kuwatia mbaroni watu 25, Mngulu alitaja majina sita pekee wakiwamo walinzi watatu, mmoja wa Mgahawa wa Vama uliokumbwa na mlipuko wa bomu Julai 7, mwaka huu.


“Tunawashikilia walinzi wawili wa Mgahawa Chinese unaopakana na Mgahawa wa Vama na mwalimu wa Shule ya Msingi Ormet wilayani Arumeru,” alisema.


Polisi pia inamshikilia wakala wa kampuni ya mabasi ambayo haikutajwa, Abdi Salim (31) na mfanyabiashara Said Temba (42).


Kitendawili
Akizungumzia kuhusu mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa Chadema katika Viwanja vya Soweto, DCI alisema hadi sasa hawajabaini aliyeingiza bomu hilo nchini.


“Kiwanda kilichotengeneza bomu lililolipuka kwenye mkutano wa Chadema Soweto kilishafungwa na hakuna kumbukumbu yoyote inayoonyesha liliuzwa kwa nani na nchi gani,” alisema Mngulu.


Licha ya kukiri kubaini kuwa bomu hilo lilikuwa la kutengenezwa kiwandani China, polisi haijafanikiwa kujua walioinunua kutokana na kukosa taarifa muhimu kutoka kwenye kiwanda husika.


Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha, Duwan Nyanda alisema watu 17 wamekamatwa na kushtakiwa kwa matukio ya milipuko ya mabomu hayo.


Alisema watu 16 wameshtakiwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio la bomu kwenye Baa ya Arusha Night Park wakati mmoja anatuhumiwa kwa bomu la Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasiti.


Kanisa lapiga marufuku vifurushi
Ili kukabiliana na matukio ya kulipuliwa kwa mabomu, Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu ya Mji mdogo wa Mirerani, Simanjiro, Manyara, imepiga marufuku waumini wake kuingia na vifurushi kanisani.


Akizungumza jana kwenye misa iliyofanyika kanisani hapo, Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Benedict Shayo alisema kamati ua utendaji ya kanisa hilo imeamua hivyo ili kuhakikisha usalama unakuwapo wakati wa ibada.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: