BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SHULE ZA SERIKALI ZILIZOFANYA VIBAYA MITIHANI YA KIDATO CHA SITA 2014 KUKIONA CHA MOTO.

WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI YA KIGURUNYEMBE ILIYOPO MANISPAA YA MOROGORO MWAKA 2012.  PICHA/MTANDA BLOG.
 
SHULE zote za Serikali zilizofanya vibaya katika matokeo ya Kidato cha Sita mwaka huu 2014, ambazo mazingira na nafasi yake iliruhusu kufanya vizuri, zimeamriwa kujieleza sababu za kufanya vibaya.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Jumanne Sagini alisema Makatibu Tawala Mkoa, wameagizwa kutoa maelezo na kufanya utafiti ndani ya mwezi kubaini sababu za shule hizo kufanya vibaya ili hatua stahiki zichukuliwe, hali hiyo isijirudie.

“Tumetaka maelezo kutoka kwa makatibu tawala Mkoa; Kwa nini shule zimefanya vibaya. Matokeo ya hovyo kama haya ni jambo ambalo haliwezi kueleweka, na wasimamizi wa elimu nimewaambia halikubaliki. “Shule kongwe kama Tambaza na Iyunga, zinazopewa fedha na Serikali, zina walimu wa kutosha, zina maabara, nyumba za walimu lakini bado matokeo yanakuwa ya hovyo hivyo, nini wanatuambia?” Alisema.

Sagini aliongeza: “Sisi wenyewe imetuudhi, imetuhuzunisha na kwa kweli haikuwa matarajio ya Serikali kwa shule kongwe kuwa na matokeo mabaya.” Hata hivyo, alisema, anazo taarifa za kuwapo kwa vikao vya kushughulikia matokeo mabaya katika Shule ya Tambaza ya jijini Dar es Salaam.

Sagini ambaye hakutaja idadi ya shule zinazotakiwa kujieleza, alisema baada ya kupokea taarifa hizo, Serikali itajua hatua za kuchukua juu ya waliopewa dhamana. Alisema tatizo lililochangia baadhi ya shule kufanya vibaya ni kukosa usimamizi makini.

Aliwataka wakuu wa shule, kutimiza wajibu wao. Wanafunzi wa Sayansi Wakati huo huo, Serikali kwa kutambua umuhimu wa masomo ya Sayansi na mwitikio chanya uliopo sasa kwa wanafunzi, imeamua wanafunzi waliofaulu masomo hayo na kupangiwa ya Sanaa, watarejeshwa katika tahasusi hizo.

Alisema wameshatoa maagizo kwa wakuu wa shule na maofisa elimu wilaya na mkoa, kuhakikisha wanafunzi waliofaulu masomo ya Sayansi na kupangiwa Sanaa, wanabadilishiwa iwapo watataka.

“Kama wanafunzi walifaulu Sayansi na kupangiwa katika tahasusi za Sanaa kutokana na kukosa nafasi, wakitaka kuendelea na Sayansi wana fursa ya kubadilisha kupitia wakuu wa shule,” alisema.

Alisema endapo tahasusi za Sayansi hazifundishwi katika shule walizopangiwa, wanafunzi husika wanaweza kuwasilisha maombi kwa maofisa elimu wa mikoa ambayo shule hizo zipo kupitia kwa wakuu wa shule walizopangiwa wabadilishwe.Jumla ya wanafunzi 22,685 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano kusoma tahasusi ya Sayansi ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi 18,746 waliochaguliwa mwaka jana.

Mabadiliko hayo ni hatua ya Serikali kutimiza lengo la kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi kuendana na Malengo ya Milenia na kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Wakati huo huo, Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili kujiunga Kidato cha Tano. Katika matokeo ya mwaka huu, wanafunzi 71,527 walikuwa na sifa za kujiunga na Kidato cha Tano kwa kupata Daraja la Kwanza hadi la Tatu.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: