BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SIRI YA MAWAZIRI KUPIGWA STOP ZIARA ZA RAIS KIKWETE WAFICUKA KATIKA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM MJINI DODOMA

 
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiagana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi kabla ya kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati kuu ya chama hicho juzi. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama. Picha na Ikulu. 


Dodoma.
Katika kile kinachoonekana kutaka mawaziri washiriki vikao vya kamati za Bunge la Katiba ili kukidhi matakwa ya akidi, Rais Jakaya Kikwete amesema hakuna ulazima wa mawaziri kuambatana naye kwenye ziara zake mikoani, badala yao wawepo makatibu wakuu wa wizara kama wanahitajika.


Rais Kikwete alinukuliwa akisema ndani ya Kamati Kuu ya CCM iliyomaliza kikao chake juzi mjini hapa kwamba yeye si kikwazo cha mahudhurio kwenye kamati za Bunge hilo na kwamba hata katika ziara yake ya Morogoro hawahitaji.


“Mwenyekiti aliweka wazi kabisa kwamba hata katika ziara yake ya Morogoro watumwe makatibu wakuu wa wizara kama kuna ulazima huo,” kilisema chanzo chetu.


Hata hivyo, katika ziara yake mkoani Morogoro iliyoanza jana, Rais Kikwete aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani ambaye pia ni Mbunge wa Ulanga Mashariki ziara hiyo ilikoanzia.


Pia alikuwapo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele ambaye alihudhuria tukio la uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini katika Kijiji cha Mwaya.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema: “Kamati Kuu inawahimiza wajumbe wa Bunge la Katiba, kuhudhuria vikao vya kamati na vile vya Bunge na kushiriki katika mijadala kwa kutanguliza masilahi mapana ya Taifa na hatimaye kuipatia nchi Katiba inayotarajiwa na Watanzania wote.


Akifafanua, Nnauye alisema suala la mahudhurio kwenye vikao lilizungumzwa kwenye CC na kwamba mawaziri na wajumbe wengine wa Bunge la Katiba, wametakiwa kupunguza utoro ili akidi ya wajumbe iwe inatimia wakati wa kufanya uamuzi.


Nnauye alisema tatizo la wabunge na mawaziri watoro katika vikao vya kamati linajulikana hata ndani ya CCM... “Sasa ni wakati wa kuwaambia kuwa wapunguze kazi zao nje ya Bunge maana suala la utoro ni kweli linatufikia na wabunge nawasihi sana wasiwe watu wa kutoka-toka wakati vikao vinaendelea,” alisema.


Akidi vikaoni
Suala la akidi limekuwa likikwaza kamati za Bunge Maalumu kiasi cha kusababisha baadhi kuchelewa kuanza kwa vikao na wakati mwingine kuahirishwa.


Kadhalika, baadhi ya ibara kwenye Rasimu ya Katiba zimekuwa zikikosa akidi ya theluthi mbili ya kura kutokana na utoro wa baadhi ya wajumbe, wakiwamo mawaziri ambao mara kadhaa wamelalamikiwa na wenyeviti wa kamati kwa kutohudhuria.


Agosti 18, mwaka huu Kamati namba 11 ililazimika kuweka kando kazi zake na ikafanya kile ilichokiita semina ya uelewa kwa wajumbe, baada ya akidi kutofikiwa.


Kamati hiyo ina wajumbe 52 baada ya kufariki dunia kwa mmoja wa wajumbe wake, Shida Salum Mohamed lakini siku hiyo idadi yao haikuwawezesha kuanza kwa kikao baada ya kupungua kwa wajumbe kadhaa kutoka Zanzibar.


Hiyo ni miongoni mwa kamati zinazoathiriwa na wingi wa mawaziri na naibu mawaziri, wakiwamo Waziri wa Kilimo na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Godfrey Zambi, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kwebwe Steven na Manaibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Adam Malima.


Pia katika kamati hiyo yumo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud na Naibu Waziri wa Mawasiliano Zanzibar, Issa Gavu.


Wengine ni Hawa Ghasia (Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi), Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu), Celina Kombani (Ofisi ya Rais – Utumishi) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Mahadhi Juma Maalim.


Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri wake wa nchi, Mohammed Aboud. Hata hivyo, haikufahamika mara moja kama walikuwa miongoni mwa waliokwaza kikao hicho.


Tatizo la akidi pia lilijitokeza juzi katika Kamati Namba Tatu kiasi cha kumsukuma, Mwenyekiti wake, Dk Francis Michael kuamua kuahirisha kikao saa tano asubuhi hadi saa nane mchana kutokana na kile alichokiita kuwapa muda wajumbe waende kusoma zaidi Sura ya Tisa ambayo inahusu muundo wa Bunge.


Dk Michael alikiri kwamba hadi ilipotimu saa 4:00 asubuhi juzi, kamati yake ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa wajumbe wanne hivyo waliwapigia simu na kubaini kwamba walikuwa katika shughuli nyingine, ikiwamo kumpokea Rais Kikwete uwanja wa ndege.


“Baadhi ya wajumbe ni mawaziri, kwa hiyo baada ya kukamilisha majukumu yao walifika na saa tano hivi akidi ilikuwa imetimia,” alisema Dk Michael.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: