BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

FEDHA ZA SIKU 60 ZA UENDESHAJI WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA MPYA ZAWACHONGANISHA SITTA NA KATIBU WAKE DODOMA.

Fedha zamgonganisha Sitta na katibu wake

Mwenyekiti wa Bunge la Katiba.PICHA|MAKTABA

Dodoma.
Kauli ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta kwamba fedha ambazo zitakuwa zimeokolewa katika siku 60 za uendeshaji wa Bunge hilo hazitarejeshwa serikalini, bali zitatafutiwa utaratibu wa namna ya kuzitumia, imemgonganisha na katibu wake, Yahya Khamis Hamad ambaye amesema “hilo ni jambo la ajabu”.


Sitta alitoa kauli hiyo juzi usiku wakati akiahirisha Bunge hilo lenye wajumbe 500 baada ya wajumbe 130 wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kulisusia tangu Aprili 16, mwaka huu.


Wajumbe hao wamekuwa wakilipwa posho ya Sh300,000 kwa siku sawa na Sh150 milioni kwa siku kwa wajumbe wote, huku Serikali ikiwa imetenga Sh20 bilioni kwa ajili ya siku 60 za uendeshaji wa Bunge hilo.


Kauli hiyo ya Sitta kuwa fedha zitakazookolewa zitatafutiwa utaratibu badala ya kurudishwa zilikotoka, iliwafanya wajumbe wa Bunge hilo kulipuka kwa furaha na kugonga meza.


Hata hivyo, katibu wa Bunge, Yahya Khamis Hamad alishangazwa na kauli hiyo ya Sitta akisema: “Mimi hayo niliyasikia lakini kwangu pia ni ya ajabu kwa sababu fedha tulizonazo hazitoshi, sasa hizo za kubaki mimi sijui.”


Katibu huyo alisema kwa sasa, Wizara ya Fedha inawapa kiasi cha fedha kwa kile tu ambacho kinahitajika na yeye anatoa taarifa serikalini kwa kiasi kilichotumika. “Mimi sijui labda yeye anajua sitaki kumsemea,” alisema.


Sitta pia aliwaeleza wajumbe hao kuwa baada ya kukabidhi Katiba inayopendekezwa, wote watakabidhiwa cheti na Rais Jakaya Kikwete.


“Cheti hicho kitakuwa na sahihi ya Rais mwenyewe kwa hiyo tutakaa kidogo kusubirisubiri Katiba iliyokamilika, haiwezi kuwa ya ovyo ovyo tu lazima iwe na viwango vizuri,” alisema Sitta na kuongeza:


“Tutachapisha nakala nyingi kila mmoja aende na waraka huo wa kihistoria nyumbani na itakuwa ni Katiba bora sana hapa Afrika na Kusini mwa Sahara.”


Mwenyekiti huyo aliwapiga vijembe viongozi wa Ukawa na makundi mengine yanayopaza sauti kutaka Bunge hilo lisitishwe ili kuokoa pesa


“Tutamaliza zoezi hilo Oktoba 3, mwaka huu ili tutoke na Katiba inayopendekezwa kinyume na wale wanaopiga kelele ovyo bila kuwa na sayansi kichwani eti unaokoa gharama kwa kusitisha mchakato.


“Mchakato huu ungesitishwa ina maana utawala ujao, rais ajaye ingembidi kuanza upya na Tume na aingie tena kwenye Bunge Maalumu la Katiba,” alisema Sitta.Lakini tukiwa na Katiba inayopendekezwa basi hilo ni tunda lililoiva atakabidhiwa Rais ajaye apeleke kwenye kura ya maoni na kazi itakuwa imekwisha na nchi inaendelea na kazi za maendeleo.


“Hapo ndiyo tunataka tufike. Tukabidhi kitu kilichokamilika, gharama yote iliyotumika tangu Tume ya Warioba (Joseph) na Bunge Maalumu itakuwa sasa imepata majibu, hakuna kilichopotea kwa sababu sasa tutakuwa tumeshapata Katiba inayopendekezwa.”


Mchakato wa Katiba mpya, unaelezwa kutafuna fedha nyingi za walipakodi huku iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikielezwa kutumia Sh69 bilioni.


Mbali na matumizi hayo, Bunge la Katiba lililoketi kwa siku 67 kuanzia Februari hadi Aprili mwaka huu lilitumia zaidi ya Sh27 bilioni wakati Bunge la sasa limetengewa Sh20 bilioni.


Matumizi hayo ni pamoja na Sh8.6 bilioni zilizotumika kukarabati ukumbi wa Bunge, miundombinu yake, mfumo wa sauti na ule wa usalama.


Hofu ya theluthi mbili


Wakati Bunge hilo likiwa katika hatua ya lala salama, kumeibuka hofu ya kupatikana au kutopatikana kwa theluthi mbili za kupitisha Katiba inayopendekezwa.


Kutokana na hofu hiyo, Sitta amewataka mawaziri na manaibu kuwapo bungeni kuanzia Septemba 29.


Abadili kanuni
Sitta alisema ikiwa wajumbe watafuata kanuni za Bunge hilo zinazotaka upigaji kura uwe ibara kwa ibara, shughuli hiyo itachukua siku zisizopungua 300 kuwahoji wajumbe 460.


“Ibara naambiwa zinakaribia 300 kwa hiyo itachukua siku moja kwa ibara moja. Na kwa ibara 300 ni siku 300; haiwezekani kabisa ni kinyume cha sheria. Tumepewa siku 60 tumalize,”alisema Sitta.


Hivyo, alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge imekabidhi suala hilo kwa Kamati ya Kanuni ili kuja na mapendekezo ya njia bora ya kupiga kura hizo ili wajumbe wahojiwe sura kwa sura.


Dk Migiro
Awali, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Rose-Asha Migiro alisema wajumbe waliosalia wanatosha kupitisha uamuzi kwa kuwa ni halali kisheria na kisiasa.


Alisema wajumbe wote wa Bunge ni 630 na kati ya hao, waliotoka ni 130, idadi ambayo ni sawa na asilimia 21 tu ya wajumbe wote.


“Wajumbe waliobaki ndani ya Bunge ni 500 sawa na asilimia 79 ya wajumbe wote na idadi hii ni pamoja na wajumbe 189 kutoka Kundi la 201 ambao wamebaki Bungeni,” alisema.


“Wajumbe wanaotoka Tanzania Bara ni 348 na kati ya hao 125 ni wanaotoka kundi la 201. Ukitazama takwimu zote hizi, wajumbe wa 201 ni sehemu ya Bunge hili,” alisema Dk Migiro.


“Kwa Zanzibar wajumbe waliobaki ndani ni 152 na kati ya hao 64 wanatokana na kundi la 201. Waliosusia Bunge kwa pande zote za Muungano hawafikii theluthi moja ya wajumbe waliobaki.”MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: