BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TEKNOLOJIA YA UMEMEJUA NAMNA INAVYOLETA NURU KATIKA NYUMBA ZA WATU MASIKINI.

Simu ikichajiwa kwenye kifaa kinachotumia umeme wa jua. 


Ilikuwa vigumu mwananchi wa kipato cha chini nchini kumiliki nyumba au kifaa chenye mfumo wa umemejua.

Mtu aliyemiliki moja ya vifaa hivyo alionekana kuwa na pesa nyingi. Hata hivyo, ufahari huo haupo tena na ulishazikwa kiasi kwamba hivi sasa wakazi wa vijijini wanavimiliki vifaa hivyo tena kwa urahisi sana.


Kwa sasa, bidhaa hizo zinazotumia seli za kusharabu jua ili kuzalisha umeme, zimeshuka bei kwa haraka kutokana na ukuaji wa teknolojia, kuongezeka kwa wazalishaji na kurekebishwa kwa sera za serikalini.


Uboreshaji huo umefanya vifaa vya teknolojia hiyo iliyogunduliwa mwanzoni mwa karne ya 19, kuwa maarufu nchini na kuvutia kampuni nyingi za kigeni zinazoleta bidhaa za aina mbalimbali zikiwemo taa za ndani, chaja za simu na redio.


Uzalishaji na usambazaji wa vifaa hivyo vya umemejua, vinavunja utamaduni wa miaka mitano iliyopita ambapo vifaa vingi vya kuzalisha nishati hiyo vilikuwa ni mifumo ya kupasha maji na paneli za umemejua zinazozalisha umeme mkubwa kwa matumizi ya viwandani na nyumbani.


Ilimlazimu mtumiaji anayetaka umemejua kuwa na mfumo madhubuti na betri kubwa zaidi ya voti 12 na N70 (uwezo wa betri) ili kukamilisha uzalishaji wa umeme wa mkondo mnyoofu (DC).


Mfumo wa DC unaozalishwa na paneli za solar ulisaidia kuwasha tu taa zilizopo kwenye mfumo wa umeme huo na kutoa huduma ya mwanga kwa wananchi wengi waliopo nje ya gridi ya umeme wa taifa.


Ili kuwasha televisheni na kuchaji simu ilihitaji kununua mashine maalumu za kuzalisha umeme wa mkondo umemegeu (AC) maarufu kama “Invetor” zisizopungua uwezo wa Wati 300 ambazo husaidia kuwasha vifaa vya kawaida vya umeme.


“Haya ni mabadiliko na maendeleo ya kawaida ya bidhaa kama mengine,” anasema Alex Lasteck ambaye ni Meneja Mwakilishi wa Kampuni ya Solar ya GleenLight nchini.


“Zamani mfumo pekee uliokuwapo wa kufunga umemejua majumbani ulikuwa mgumu na ghali… pia ni vigumu kwa maskini kuumudu kulipia Sh4 milioni au Sh5 milioni.


“Lakini kwa sasa taa au tochi ya sola unapata kuanzia Sh20,000 na inakidhi mahitaji hadi ya familia za hali ya chini,” anasema.


Lasteck anasema kuwa Watanzania wanatakiwa kuchangamkia teknolojia hiyo kwa kuwa asilimia 90 ya nchi haipati umeme wa gridi ya taifa.


“Ni umeme wa bei rahisi sana. Mtu anaweza kuwekeza fedha ya miezi mitatu ya kununua mafuta ili kununua taa nzuri ya umemejua ambayo itadumu kwa miaka mitano.


“Hii inawezekana kwa kuwa kila nyumba hutumia wastani wa Dola za Marekani 10 (Sh16,500) kununua mafuta ya taa kwa mwezi na baada ya miezi mitatu atakuwa na Dola 30 (Sh49,500) ambayo atapata kifaa cha muda mrefu kinachomsaidia na kuchaji simu zake,” anasema mtaalamu huyo.


Ni nishati salama
Anasema kuwa mtu anayetumia umemejua yupo salama asilimia 100 kuliko yule anayetumia mshumaa kumulika nyumba yake kwani muda wowote ajali ya moto inaweza kutokea.


Hali kadhalika nishati hiyo ni rafiki kwa mazingira kwani haitoi moshi kiasi cha kuokoa wengi kupata maradhi katika mfumo wa upumuaji.


“Kwa mfano, katika bidhaa nyingi unaweza kuchaji simu yako kupitia taa za umemejua…kwa kutumia bidhaa hizi unaweza kuchaji simu za kisasa (Smartphones) na vipakatishi (tablets) bila matatizo,” anabainisha.


Kampuni nyingi za umemejua ulimwenguni kama Sharp, Gleenlight, Cadanian Solar, Kyocera, Suntech, Yingli Green Energy na nyinginezo zimetumia fursa ya mahitaji ya watu maskini na ukuaji wa teknolojia kutengeneza taa za umemejua za teknolojia ya LED zenye sehemu ya kuchaji simu na aina mbalimbali za chaja.


Asilimia kubwa ya taa hizo zina viwango vya ukali wa mwanga ambapo ule wa juu zaidi unafanya betri ikae kwa saa 17, wa kati saa 25 na mwanga wa chini kwa saa 37.


Pia, mpango wa Serikali kupunguza kodi na tozo katika uingizaji wa bidhaa za sola na kazi ya Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), vinatoa mwanya kwa Watanzania kutumia fursa hiyo zaidi ya kutumia nishati hiyo na kuepukana na tatizo la ukosefu wa umeme linaloikabili nchi.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: