BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MARAIS WAWILI WA ZAMBIA WAFARIKI DUNIA NDANI YA MIAKA SITA, SASA ZAMBIA INAONGOZWA NA MZUNGU.


Kaimu Rais wa Zambia , Dk Guy Scott akisalimiana na maafisa wa ngazi ya juu wa vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi hiyo, mjini Lusaka jana baada ya kushika wadhifa huo kutokana na kifo cha Rais Michael Sata aliyefariki dunia akiwa nchini Uingereza alipokuwa akipatiwa matibabu, katika hospitali ya King Edward VII. Picha na AFP


London, Uingereza.
Rais wa Zambia, Michael Sata amefariki dunia nchini Uingereza, tukio ambalo limeweka rekodi nchini humo kwa marais wawili kufariki dunia wakati wakiwa madarakani huku Mzungu ambaye ni Makamu wa Rais, Dk Guy Scott akitangazwa kuwa kaimu rais.


Zambia inakuwa taifa la kwanza Afrika kupoteza viongozi hao wakiwa madarakani katika kipindi kizichozidi miaka sita tangu alipofariki Levy Mwanawasa mwaka 2008 akiwa Ufaransa.


Taarifa zilieleza kuwa Sata alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu kutokana na maradhi ambayo hayakutajwa. Lakini taarifa nyingine zinaeleza kuwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo.


Runinga ya Muzi na Gazeti la Zambia Report pamoja na tovuti mbalimbali za nchi hiyo zilieleza kuhusu msiba huo na kufafanua kuwa kamati mbalimbali za serikali hiyo zinatarajia kukutana kwa ajili ya mipango ya mazishi.


Sata (77), alifariki dunia katika Hospitali ya King Edward V11 ingawa msemaji wa hospitali hiyo hakuweza kuzungumza chochote kuhusu kilichosababisha kifo chake.


Kaimu Rais

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Zambia mwenye asili ya Uingereza, Dk Guy Scott ametangazwa kukaimu nafasi ya urais.


Waziri wa Ulinzi wa Zambia, Edgar Lungu alisema uchaguzi wa rais wa nchi hiyo utafanyika ndani ya siku 90 baada ya kutokea kwa msiba huo.


Lungu alisema Sata alifariki dunia wakati mkewe na mtoto wake wa kiume wakiwa pembeni ya kitanda alipokuwa amelala.


Kutokana na hali hiyo, Dk Scott atakuwa rais wa kwanza Mzungu Afrika tangu wakati wa utawala wa Rais wa Afrika Kusini, FW de Klerk wakati wa ubaguzi wa rangi.


Balozi wa Zambia nchini

Akizungumzia kifo hicho, Balozi wa Zambia nchini, Judith Kapijimpanga alisema Sata alikuwa ameenda Uingereza kwa matibabu ya kawaida. Alisema utaratibu wa mazishi bado haujatangazwa. Alisema huenda marehemu akazikwa katika Makaburi ya Embassy Park jijini Lusaka walipozikwa watangulizi wake.


Alisema Ubalozi wa Zambia nchini umeandaa misa itakayofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Peter, Ijumaa. Taratibu za utoaji wa rambirambi zitatolewa baadaye.


Oktoba 19 mwaka huu, Rais Sata alikwenda Uingereza kwa ajili ya matibabu akisindikizwa na mke wake pamoja na baadhi ya ndugu wa familia ingawa haikuwekwa wazi.


Kwa muda mrefu, Sata alikuwa hajaonekana hadharani tangu alipotoka katika mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa (UN) ambako alishindwa kuhutubia mkutano huo kutokana na kuugua ghafla akiwa hotelini New York, Marekani.


Siku chache kabla ya tukio hilo alihudhuria mkutano wa ufunguzi wa Bunge jijini Lusaka huku akitania kwa kusema ‘sijafa’.


Tiba nchini Israel

Wasiwasi kuhusu afya ya Sata, ulianza kutanda Juni baada ya kutoonekana kwenye shughuli mbalimbali za kiserikali bila ufafanuzi wowote. Hata hivyo, siku chache baadaye iliripotiwa kuwa alikwenda Israel kwa ajili ya matibabu.


Kikwete atoa salamu
Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Makamu wa Rais wa Zambia, Dk Scott kufuatia kifo hicho.


Rais Kikwete alisema: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi, habari za kifo cha Michael Sata kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, na kwa niaba yangu mwenyewe, nakutumia salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu na kupitia kwako kwa familia ya wafiwa na ndugu wa hayati Sata pamoja na wananchi wote wa Zambia.”


Kikwete alisema hayati Sata atakumbukwa daima kwa sababu alikuwa mmoja wa viongozi wa kuigwa Afrika kutokana na kuwaletea wananchi wake maendeleo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: