BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VIRUSI VYA EBOLA VYAWATIA HOFU WANANCHI, MJI WA MOSHI WAWA MJI WA KWANZA KUKUMBWA NA TAHARUKI TANZANIA.

http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/10/shirimatunda.jpg
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amewaondoa hofu wakazi mji wa Moshi kutokana na taharuki iliyoukumba mji huo ya kuwapo mgonjwa anayehisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa hatari wa Ebola.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini hapa jana, RC Gama alisema ni kweli Ofisi ya Afya Manispaa ya Moshi ilipata taarifa za mgonjwa ambaye anahitaji matibabu kutokana na homa kali aliyokuwa nayo.

“Mgonjwa huyo (jina tunalihifadhi), ambaye ana umri wa miaka 37, alihitaji matibabu kutokana na homa yake kutopata nafuu tangu alipopata matibabu na Manispaa ya Moshi ilimpokea mgonjwa huyo ambaye ana historia ya kusafiri katika nchi za Afrika Magharibi ambako ugonjwa huo umeenea,” alisema.

Gama, aliongeza kuwa mgonjwa huyo mzaliwa wa Marangu wilayani Moshi, mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam ambaye amewahi pia kuzuru nchi za Asia, alifika mjini hapa akitokea Dar es Salaam na ilionekana kuwa na homa kali ambapo alitengewa eneo maalum la matibabu.

“Damu ya mgonjwa huyo imechukuliwa na kupelekwa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo hatua za kina zitafuata kwa kuipeleka Nairobi Kenya, kisha kurudishwa hapa na itakapofika tu, nitaujulisha umma matokeo yake, lakini kwa sasa mgonjwa huyo anaendelea kupewa matibabu hapa,” alisema.

Tanzania Daima ilishuhudiwa mgonjwa huyo aliyefika Zahanati ya Iwa Kirua-Vunjo akipewa matibabu katika eneo alilohamishiwa la Zahanati ya Shirimatunda ambako utoaji huduma ulisitishwa kwa muda hadi sasa ili kumhudumia na madaktari walikuwa wame valia mavazi maalum ya kujikinga na Ebola.

Hata hivyo kumetokea sintofahamu ya uamuzi wa kituo cha Shirimatunda kuwekwa kama eneo maalum la kutolewa huduma kwa mgonjwa atakayeonekana kuwa na Ebola.

Kutokana na uamuzi huo, Diwani wa Kata ya Shirimatunda, Felix Mushi, aliushutumu uongozi wa Manispaa ya Moshi kwa kutenga eneo hilo kwa ajili ya wahanga wa Ebola huku kukiwa ni makazi ya watu.

Mkuu wa Seminari ya Don Bosco inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, Augustine Sellam, alisema seminari hiyo ina kundi kubwa la wanafunzi wanaosoma hapo, hivyo inashangaza kuona ‘karantini’ hiyo inawekwa karibu na eneo hilo.

Alisema mazingira hayo yanawaweka wanafunzi katika hofu ya kukubwa na Ebola na kuwaathiri kisaikolojia.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Mtumwa Mwako, alisema kituo cha Shirimatunda kimewekwa kwa ajili ya tahadhari ya watu wanaohisiwa kuwa na Ebola.

Dk. Mwako, aliongeza kuwa pia wataalamu wanaomhudumia mgonjwa huyo, nao wamewekwa katika karantini hadi hapo sampuli za vipimo zitakaporejea na kubaini mgonjwa huyo anasumbuliwa na ugonjwa gani.

Aidha, pamoja na kwamba bado majibu ya vipimo vya mgonjwa huyo hayajatolewa, lakini ametahadharisha wananchi kupunguza salamu za kupeana mikono na kukumbatiana ili kuepusha zaidi athari za ugonjwa huo kama utaingia mkoani hapa.TANZANNIA DAIMA
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: