BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KISA CHA ALBINO KUAMUA KWA MAKUSUDI KUMTWANGA MAKONDE KIONGOZI WAO, IKULU YA RAIS DK JAKAYA KIKWETE.

 

Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania, Ernest Kimaya (kushoto) akizuiwa asiendelee kugombana na wanachama wake karibu na uzio wa Ikulu waliokuwa wakitaka wote waambatane kwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete kueleza matatizo yao jijini Dar es Salaam jana. Rais Kikwete alitoa mwaliko wa kukutana na viongozi wa chama hicho. Picha na Anthon Siame.


Dar es Salaam.
Hali ya sintofahamu ilitokea jana baada ya wanachama wa Chama cha Albino Tanzania (Tas) kumshambulia kiongozi wao, Ernest Kimaya wakati wakiwa njiani kuelekea Ikulu ambako Rais Jakaya Kikwete aliwaita kwa mazungumzo.



Pembeni ya barabara inayopakana na Ikulu, karibu na jengo la Wizara ya Elimu wakati wakielekea kumuona Rais Kikwete, wanachama hao walianza kumshambulia Kimaya wakidai kuwa si kiongozi halali, lakini aliokolewa na maofisa usalama waliokuwapo katika tukio hilo.


Wanachama hao walitaka kushinikiza na wao kumwona Rais Jakaya Kikwete badala ya viongozi 15 ambao ndiyo waliotakiwa wamwone Rais na kuzungumza naye. Saa moja baadaye, viongozi hao wa Tas waliingia Ikulu kuonana na Rais Kikwete.


Wanachama hao walikuwa wakimtaka Kimaya aachie wadhifa wake kwa kuwa si kiongozi.


Kimaya alizomewa muda wote na kumvuta nguo na baadhi ya wanachama hao ambao walimtuhumu kuwa anajinufaisha na vifo vya albino vinavyozidi kutokea nchini.


Hata hivyo, Kimaya alishindwa kujizuia na kutaka kupigana na baadhi watu waliokuwa wakimzonga na kumtukana. Maofisa usalama walimchukua na kumwondoa eneo la tukio ili vurugu zisiendelee.


Baadhi ya wanachama wa Tas walisema viongozi wao wamejikusanya wenyewe kwenda Ikulu bila kuwashirikisha na kuwa hawafanyi mikutano ya mara kwa mara zaidi ya kuwaita kwenye maandamano.


Mmoja wa albino hao, Nuru Iddi alisema hawana imani na viongozi wao kwa sababu muda wao wa kuwepo madarakani uliisha tangu mwaka jana.


Alisisitiza kuwa tangu wakati huo hawajafanya uchaguzi wowote na viongozi wametulia ili waendelee kujinufaisha.


“Albino akiuawa kule Mwanza mimi ndiyo napata uchungu, siyo hawa viongozi... wao wanapokea michango mingi kutokana na vifo vya wenzetu lakini hawafanyi jambo lolote la maana kulinda maisha yetu,” alisema mwanachama huyo.


Iddi aliongeza kuwa wao ndiyo walitakiwa kuonana na Rais Kikwete ili wamueleze hali halisi na nini cha kufanya ili kulinda maisha yao.


Aliulaumu uongozi wa Tas kwa kutowashirikisha wao kama wanachama kutoa maoni ambayo yangewasilishwa kwa Rais.


Naye Mwalimu Matimbwa alisisitiza kuwa viongozi wao wako nje ya muda kikatiba. Alisema mwaka 2006 kulikuwa na kisa kimoja tu cha mauaji ya albino lakini mpaka sasa idadi imefikia 78. Aliushutumu uongozi wa Tas kutodhibiti ongezeko hilo la mauaji ya albino.


“Nasikia uchungu sana ninapoona wenzangu wanauawa lakini baadhi yetu wanajinufaisha na mauaji hayo. Hatuwezi kushinda vita hivi kama hatuna uongozi thabiti. Tunataka uchaguzi ufanyike haraka sana,” alisisitiza Matimbwa.


Matimbwa aliongeza kuwa katiba yao inataka uchaguzi ufanyike kila baada ya miaka mitano lakini uchaguzi huo haukufanyika mwaka jana.


Kimaya alikiri kuwa walitakiwa kufanya uchaguzi mwaka 2014, lakini walikubaliana na wanachama kuwa uongozi uliokuwepo madarakani kwa ngazi ya wilaya, mikoa na taifa uendelee na kazi.


“Sisi tupo madarakani kihalali kwa sababu wanachama wenyewe ndiyo walipendekeza kuwa tuendelee kuongoza. Hili ni kundi la wahuni tu, siyo wanachama wetu,” alisema kiongozi huyo kabla ya kushambuliwa na wanachama waliokuwa wakipiga kelele wakisema “hatumtambui, aachie kiti huyo”.


Kimaya alifafanua kuwa mara ya mwisho walifanya uchaguzi mwaka 2009, lakini mwaka jana walishindwa kufanya uchaguzi kwa sababu kulikuwa na mwingiliano wa mambo.


Rais Kikwete aliandaa chakula cha mchana na viongozi wa Tas, Ikulu jijini Dar es Salaam. viongozi wa Tas walipata nafasi ya kuongea naye juu ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanayoshika kasi nchini kwa sasa.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: