BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SERIKALI IMELALA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI ?.

http://www.theeastafrican.co.ke/image/view/-/2064462/medRes/618217/-/maxw/600/-/719dacz/-/kikwete.jpg
RAIS DK JAKAYA MRISHO KIWETE.

Mwaka 1994, niliulizwa swali hili nilipofanyiwa usaili wa kazi katika ofisi za Shirika la Chakula Duniani (FAO), jijini Rome nchini Italia. Jibu nililotoa halikukubalika.


Swali lilikuwa: “Kuna mgogoro Morogoro, hususan Mvomero, kati ya wakulima na wafugaji, tupe ufumbuzi ndugu msomi ?’’.


Mimi nikajibu: “Siyo rahisi kwani kama jipu, Serikali yetu imejihusisha kwa kiasi kikubwa kupunguza wingi wa usaha badala ya kutokomeza kiini cha jipu lenyewe!’’


Jamaa wakanijibu na kunieleza hivi: “Kafanye utafiti ndipo utujibu kama kuna utata kama huo.’’


Miaka 20 baadaye, Desemba 2014, Joel Bendera akiwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro alielezwa na mwandishi wa habari kuwa kuna moto Mvomero.


Bendera alijibu kuwa huo ni moshi unaofuka, kwani moto alishauzima zamani.


Siku iliyofuata barabara kuu itokayo Morogoro kwenda Iringa ilifungwa na wakulima wa Dumila kwa sababu wafugaji waliwazuia wakulima kuandaa mashamba yao. Mabomu ya moshi yakapigwa, maisha ya watu yakapotea tena!


Morogoro si shwari
Hali bado siyo shwari Morogoro! Hali ni tete na inahitaji ufumbuzi wa kina. Serikali imemhamisha Mkuu wa Mkoa Bendera na sasa yuko Manyara.


Swali ni je, aliyeteuliwa kwenda Morogoro analo jibu la mgogoro huu? Katika mgogoro kati ya wakulima na wafugaji hasa katika Wilaya ya Mvomero, mimi nimebaini yafuatayo:


Mosi, kuwapo kwa sera za wanyama pori zinazotawala, yaani mwenye nguvu mpishe. Haya ndiyo maisha ya kila siku.


Pili, kuna mbinyano wa binadamu, mazao na mifugo kunakozidi viwango vya kisayansi.


Mbinyano huu unasababisha ukosefu wa makazi bora, mashamba salama ya kulima, malisho bora ya mifugo na uhaba wa majisafi kwa shughuli zote za kilimo na ufugaji.


Tatu, ongezeko la uhasama kati ya wafugaji na wakulima, hali inayomaanisha kwamba hakuna amani Mvomero na mkoa wa Morogoro kwa jumla.


Nne, kukosekana kwa imani kati ya viongozi na wananchi katika ngazi zote. Serikali Kuu haina budi kurudisha na kudumisha amani hiyo.


Tano, Kuna dalili kuwa binadamu hana thamani tena mbele ya ng’ombe. Haya ndiyo yanayotokea Mvomero na maeneo mengine nchini.


Masuala ya kurekebisha
Tutaendelea na hali hii mpaka lini? Yapo mambo yanayopaswa kufanyiwa kazi ikiwamo kuwa na uwiano wa ardhi dhidi ya mifugo na mimea. Hili ni suala kisayansi.


Wataalamu wafanye hesabu za uwiano huo na kuwahusisha kielimu wakazi wote, viongozi na wageni.


Makundi yote haya yaelimishwe kuhusu takwimu na viwango uwiano huo. Sayansi hupingwa kisayansi siyo kwa mikuki au bunduki na mabomu ya machozi kama ilivyo sasa.


Hili ni suala la kufanyiwa kazi kisayansi na wala siyo siasa mbovu isiyo na tija.


Elimu zaidi itolewe ili wafugaji wathamini ubora badala ya uwingi. Kwa mfano, ikiwa ng’ombe mmoja wa nyama anaweza kunenepeshwa akafika kilo 1,000, kuna haja gani ya kuhangaika na ng’ombe 1,000 kwenye ekari moja ya ardhi?


Wengi hawajui kama ng’ombe mmoja bora wa maziwa anaweza kutoa lita 100 za maziwa kwa siku! Tutembelee Kenya, Botswana na Israeli, haya yanafanyika huko.


Kinga ni bora kuliko tiba. Kuna mila potofu ya Kiafrika, eti mtu azae watoto wengi ili wengine wakifariki wachache watakaobaki watamsitiri uzeeni.


Mila hii imeshamiri kwa wafugaji. Hawajui kuwa ikiwa mtu atafuga kiwango mwafaka cha mifugo kwa ekari, huduma za malisho, maji na tiba zitamudu uzalishaji bora.


Katika migogoro mingi ya wakulima na wafugaji, wengi hawajui kuwa mara nyingi mchokozi huwa ni mfugaji. Mimi naamua kumfunga paka kengele kwa kusema ukweli.


Serikali isilionee aibu suala hili. Wafugaji waende na wakati na wafuge kwa njia za kisasa.
Inasikitisha kuwa wanaofuga bila viwango wapo wanasiasa hivyo nao wanazidi kuchochea utambi.


Tujifunze kwa wengine
Tujifunze kutoka katika baadhi ya nchi kama vile Kenya, Botswana na nchi za Ulaya. Kenya ardhi yote imegawiwa na imewekewa uzio, kiasi kwamba wafugaji wana nafasi ndogo sana ya kuzurura na mifugo yao na kuwabugudhi wakulima.


Nchini Botswana, kila ng’ombe ana kitambulisho na Serikali imeweka vizuizi na senyenge kati ya wilaya na kati ya mikoa, hivyo mifugo hairuhusiwi kuvuka vizuizi hivi bila ruhusa ya Serikali.


Jambo hili linafanya pia magonjwa yasienee kienyeji na ndiyo maana nchi hiyo inauza nyama Ulaya. Tanzania tunaizidi Botswana kwa wingi wa ng’ombe lakini tumepigwa marufuku kwenye soko la kimataifa!


Kwa nchi za Ulaya, idadi ya mifugo ambayo mfugaji anaweza kufuga hasa ng’ombe, lazima iwe na kibali cha serikali ya wilaya husika. wilaya ndizo zinazohusika na huduma zote za matibabu lakini kwa gharama za mfugaji.


Viongozi wa wafugaji, wakulima na Serikali, watembelee kwa pamoja kuona mifano iliyotajwa hapo juu. Elimu ya kuona ni bora kuliko ile ya kusikia.


Tuwasikilize wananchi
Siasa zimeshindwa katika suala hili, je, wananchi wao wanasemaje? Nitoe maoni ya baadhi ya Watanzania waliowahi kuzungumzia kuhusu dawa ya tatizo hili.


Kim Niuyai anasema: “Ardhi ipimwe igawiwe kwa wananchi. “Maeneo kwa ajili ya kilimo na ufugaji yabainishwe na yatenganishwe. Tuweke miundombinu kama maji na majosho katika maeneo ya wafugaji. Pia elimu itolewe kwa wafugaji kuhusu ufugaji bora na wenye tija, Serikali ilete mbegu bora itakayotuezesha kufuga mifugo michache, lakini yenye faida.”


Baraka Mfilinge anasema: “Binafsi naamini suluhu ya tatizo hili kubwa hapa nchini ni kupima ardhi yote na kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji kwa kutoa hati miliki. Kwa sasa takwimu zinaonyesha ni asilimia kumi ya ardhi yote Tanzania ndiyo pekee imepimwa, hali inayosababisha migogoro mingi.”


Naye Richard Mramba anasema: “Viongozi wa Serikali wa eneo husika, wakiacha kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji tatizo litakwisha. Maana haiwezekani mkulima ajipinde kulima mazao kama mahindi, halafu yanapokaribia kuvunwa, mfugaji anapeleka mifugo yake kulisha kwenye mazao hayo.’’


Nuru Rashid anasema: “Tatizo la ardhi linatatulika bila kumwaga damu. Ni kugawa maeneo kulingana na mahitaji na kuweka sheria kati yao. Tatizo la viongozi wetu hawana mwamko wa maendeleo, wanajiwazia wao na familia zao, ndiyo maana hata nchi zisizo na maeneo zinatupita kimaendeleo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: